Halmashauri yathitisha wagombea ubunge

Wawania uwakilishi Z’bar wawekwa kiporo

NA SAIDA ISSA, DODOMA

MWENYEKITI wa Chama cha Mapinduzi (CCM), ambaye pia ni Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. John Magufuli, amesema kamati kuu ya chama hicho, imefanya kazi kubwa ya kupitia na kuchambua taarifa za wagombea walioomba nafasi za ubunge kupitia chama hicho.

Dk. Magufuli alieleza hayo jana jijini Dodoma wakati akifungua mkutano wa halmashauri kuu ya CCM kilichokuwa na ajenda ya kupitisha majina ya walioomba nafasi ya ubunge kupitia chama hicho.

Alisema majina ya wagombea hao yalijadiliwa kwa siku mbili kuanzia ngazi ya kamati ya usalama na maadili na baadae mjadala huo kufikishwa katika kikao cha kamati kuu ya halmashauri kuu ya CCM.

Alisema vikao hivyo vilifanya uchambuzi wa kina kwani walitumia taarifa kutoka katika vyanzo mbalimbali ili kujiridhisha na sifa za mgombea atakayeteuliwa na kueleza kuwa kama yupo mtu ana ufafanuzi wa taarifa za mgombea taarifa za kutosha zipo.

“Kamati kuu ilikaa na kujadili vizuri sana ili kurahisisha kazi itakayofanyika, hiyo ni sababu hakutakuwa na upendeleo wa mtu wala kumnyima mtu haki yake, sababu kila mtu ana haki yake”, alisema Dk. Magufuli.

Alikieleza kikao hicho kwamba ilikuwa lazima kutumia taarifa nyingi na kuwajadili wagombea kwa muda mrefu ili watakaopitishwa wawe watu wenye uwezo wa kuipeperusha vyema bendera ya chama hicho na kujipatia ushindi kwenye uchaguzi mkuu.

Mwenyekiti huyo alibainisha kuwa nafasi walizoomba wagombea hao ni nyeti na ilikuwa lazima kujiridhisha katika majina hayo kwani kati yao ndipo watakapopatikana mawaziri na manaibu, waziri mkuu, spika na naibu spika.

“Wawe na sifa za kuwa viongozi na wanafahamu dira na sera ya chama, kazi kubwa ilifanywa na kamati kuu hivyo kamati ya usalama na kamati kuu zimejitahidi kuchagua na kupata viongozi wenye sifa na wazalendo, wenye sifa za kuwa viongozi na wenye uwezo wa kuwasimamia wananchi”, alisema.

Aliwataka wajumbe wa halmashauri kuu kujadili mapendekezo kwa umakini mkubwa na kutanguliza mbele maslahi ya chama na taifa na si undungu, urafiki wala udini, bali uwezo wa mtu kuongoza kwani ndio msingi wa chama na ndio misingi iliyoachwa na waasisi wetu.

Katika hatua nyengine, Mwenyekiti huyo aliwashukuru wajumbe wa halmashauri kuu ya Taifa kwa kumpigia kura kwa wingi kwenye mkutano mkuu wa chama hicho uliompitisha kuwa mgombea wa urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

“Napenda niwashukuru kwa kazi zenu na juhudi zenu nilipozunguka na kutuma waliokuwa wananiwakilisha kwa ajili ya kupata wadhamini mikoani kwenu katika wadhamini kwa ajili ya kutimiza masharti ya NEC”, alisema.

Kwa upande wake Katibu Mkuu chama cha Mapinduzi CCM, Dk. Bashiru Ally alisema kuwa wajumbe wa kamati kuu na wajumbe wa halmashauri kuu katika kikao cha mwisho cha CCM kinachotakiwa kufanya uteuzi wa wawagombea wa nafasi za ubunge na nafasi za uwakilishi kwa ajili ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2020

Alisema kuwa kutokana na ratiba ya tume za uchaguzi za NEC na ZEC kupishana katika hatua ya uteuzi kikao hakitafanya uteuzi wa wawakilishi na badala yake kazi hiyo uteuzi utafanya kwa ubunge na viti maalum ubunge.

Akitangaza majina ya waliopitishwa kugombea nafasi ya ubunge kutoka Zanzibar, Katibu wa CCM itikadi na uenezi Humphrey Polepole alimtaja Abdallah Rashid Othman (Pandani), Juma Shaaban Juma (Wete), Juma Usonge Hamad (Chaani), Yahya A. Khamis (Kijini) na Khamis A. Vuai (Mkwajuni).

Wengine ni Simai H. Sadik (Nungwi), Juma O. Hija (Tumbatu), Mbarouk J. Khatib (Bumbwini), Soud M. Juma (Donge), Abdullah A. Hassan (Mahonda), Ramadhan S. Ramadhan (Chake Chake), Juma M. Juma (Chonga) na Juma H. Omar (Ole).

Wengine ni Khamis K. Ali (Wawi), Ahmed J. Ngwali (Ziwani), Moh’d A. Mwinyi (Chambani), Rashid A. Rashid (Kiwani), Prof. Makame Mbarawa (Mkoani), Khamis S. Suleiman (Mtambile), Haji M. Mlenge (Chwaka), Khalifa S. Suleiman (Tunguu) na Khamis H. Khamis (Uzini).

Wengine ni Ravia I. Faina (Makunduchi), Jaffar Sanya Jusa (Paje), Mustafa Mwinyikondo (Dimani), Abass Ali Hassan (Fuoni), Moh’d M. Ali- (K/samaki), Kassim H. Haji (M/kwerekwe), Haji Amour Haji (Pangawe) na Mwantakaje H. Juma (Bububu).

Wagombea wengine Zubeida Kh. Shaibu (Mfenesini), Abdulghafar Idrisa (Mtoni), Zahor M. Haji (Mwera), Maulid Saleh Ali (Welezo), Mussa H. Mussa (Amani), Ussi S. Pondeza (Chumbuni) na Mwanakhamis K. Said (Magomeni).

Wengine ni Salum H. Abdullah (Mpendae), Ali Juma Moh’d (Shauri moyo), Ali Hassan Omar (Jang’ombe), Hamad Masauni Yussuf (Kikwajuni), Ahmada Y. Abdulwakil (Kwahani) na Moh’d S. Omar (Malindi).