Abainisha vipaumbele
Aahidi kuijenga Z’bar mpya
NA KHAMISUU ABDALLAH
MGOMBEA wa urais wa Zanzibar kwa tiketi ya Chama cha Mapinduzi, Dk. Hussein Mwinyi, amewataka viongozi wa CCM wa ngazi zote kufanyakazi usiku na mchana ili kuhakikisha chama hicho kinashinda kwenye uchaguzi mkuu.
Kauli hiyo aliitoa jana alipokuwa akizungumza na wanaCCM katika ofisi ya CCM Kisiwandui, mara baada ya kuchukua fomu ya kugombea nafasi hiyo katika ofisi za Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC) zilizopo Maisara.
Alisema baadhi ya wanaCCM wamekuwa na tabia ya kubweteka wakidhani kwamba ushindi unaweza kupatikana kwa urahisi, hivyo kila mmoja ahakikishe anawajibika kwa eneo lake kuhakikisha ushindi kwenye uchaguzi.
Dk. Mwinyi aliwataka viongozi wote wa ngazi ya mashina, mabalozi, watendaji wa matawi, wadi, majimbo, wilaya hadi ofisi kuu ya chama kuhamasisha wananchi kujitokeza kwa wingi siku ya kupiga kura.
Aidha alisema hana mashaka na viongozi wa ngazi hizo kwani jukumu hilo wanaweza kulitekeleza kwa ufanisi mkubwa na wakilitekeleza kwa dhati basi CCM itashinda kwa asilimia kubwa.
Alisema, anafahamu kuwa wananchi na wanaCCM wa Zanzibar wana matumaini makubwa na yeye hivyo aliwahakikishia kwamba ameamua kugombea nafasi hiyo kwa dhamira moja ya kuwatumikia wazanzibari.
“Sikugombea ili nije kujaribu, lakini nilijipima na uwezo nnao, nahitaji ushirikiano kutoka kwenu ili niweze kuijenga Zanzibar mpya yenye matumaini makubwa kuweni na matarajio na tutayatimiza”, alisema.
Akizungumzia vipaumbele baada ya kuchaguliwa alisema ataondosha matabaka ikiwemo U-pemba na U-unguja na u-kusini na u-kaskazini na tabaka za kidini ili wananchi wote wawe wazanzibari na wanufaike na nchi yao.
Kwa upande wa uchumi Dk. Mwinyi alibainisha kuwa atahakikisha anajenga uchumi wa kisasa ambao utaibua ajira ambazo zitawasaidia vijana.
Mbali na hayo, alisema katika kipindi cha uongozi wake ataipa kipaumbele sekta ya utalii kwa kuongeza idadi ya watalii wanaoingia nchini kutoka watalii 530,000 wanaongia nchini hivi sasa na wanzanzibari wananufaika na sekta hiyo.
Kuhusu sekta ya bandari alisema atahakikisha Zanzibar ina bandari ya kisasa itakayoweza kutoa ajira na kuleta biashara sambamba na sekta ya uvuvi wa bahari kuu maji madogo na kufuga samaki.
Hata hivyo, alisema umefika wakati kwa Zanzibar kuwa Zanzibar ya viwanda na kujenga miundombinu imara na kumalizia miradi yote iliyoanzwa na serikali ya awamu ya saba na miradi mipya na kuhakikisha maendeleo yanakuwa kwa haraka.
Dk. Mwinyi akizungumzia huduma za jamii ikiwemo afya, elimu maji na umeme, alisema ataweka mkazo katika maeneo hayo ili kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora.
Alisema ilani ya CCM inaelezea kutengeneza ajira zisizopungua 300,000 hivyo matumaini yake makubwa idadi hiyo kuongezeka ikiwa watazuia uvujaji wa mapato ya serikali.
Alisema serikali ya awamu ya nane haitakuwa na msamaha kwa watu wasiolipa kodi kwani kodi inayokusanywa ndio inayotumika katika kuwapatia wananchi maendeleo.
Kuhusu rushwa Dk. Mwinyi alisisitiza kuwa hatakuwa tayari kuvumilia wala kufumbia macho vitendo vya rushwa na badala yake ataipiga vita kwa nguvu zote.
“Nimeshasema kwa hili sitamuonea muhali mtu yoyote anaekula rushwa, mzembe na mbadhilifu wa mali ya umma na wanaofanya matumizi mabaya ya fedha za umma wajue hao ndio maadui zangu,” alisisitiza.
Alisema kila mtu ana wajibu wa kuwajibika hivyo aliwatahadharisha wale wote waliopewa madaraka wasiowajibika na kubainisha serikali ya awamu ya nane haina haja nao.
Hivyo, aliwaomba wananchi kushirikiana pamoja na kuwa tayari kuijenga Zanzibar mpya ya uchumi na wanaweza kufanya hivyo ikiwa hawataoneana muhali.
Kwa upande wake Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar, Dk. Abdalla Juma Sadala, alisema ustahamilivu, uvumilivu, upendo na mshikamano ndio kitu pekee kitakachowafikisha CCM kwenye ushindi.
Alisema Dk. Mwinyi atakapoingia madarakani atafanya maendeleo kwa vitendo kama alivyofanya Dk. Ali Mohamed Shein katika visiwa vyote vya Unguja na Pemba na visiwa vyengine vidogo vidogo.
Mbali na hayo, alimuhakikishia mgombea huyo kuwa vijana wa Zanzibar wana matumaini makubwa na uongozi wake hivyo watahakikisha wanaisimamia ilani ya CCM kifungu 1 a ibara ya 5 ni kuhakikisha inaendelea kushinda katika nafasi zote kuanzia udiwani hadi urais na tayari wamejipanga kwa hilo.
Mgombea huyo aliingia Tume ya Uchaguzi Zanzibar ZEC majira ya saa 8:52 akishindikizwa na viongozi mbalimbali wa chama wakiwemo wenye viti wa mikoa, wilaya, wazee na viongozi wengine na kukabidhiwa fomu ya kugombea urais.