NA MWANTANGA AME

MGOMBEA Urais kwa Chama cha Mapinduzi, Hussein Ali Hassan Mwinyi, amewataka wananchi kukaa mkao wa kula mambo mazuri yatayotokana na kufungua fursa nyingi za uchumi kwa kufanya mabadiliko kwa kuongeza sekta nyengine zitazosababisha makusanyo ya kodi kuongezeka.

Hayo aliyasema jana wakati akizungumza na ZBC TV, katika kipindi maaluum ambapo alisema atayafanya hayo ikiwa ni sehemu itayofungua fursa za kibiashara huru, ili kodi iweze kukusanywa vilivyo, kwa vile wananchi wa Zanzibar wanahitaji maendeleo.

Alisema Zanzibar hivi sasa inafanya utafiti wa kupatikana kwa raslimali ya mafuta na gesi asilia, lakini utapokamilika  na kuanza kuchimbwa atahakikisha inawanufaisha wananchi wa hapa nchini, ili kukuza kipato chao na uchumi wa nchi.

Alisema Uchumi wa Zanzibar hivi sasa umekuwa unategemea Utalii na Karafuu, lakini atapokuwa madarakani atahakikisha sekta nyengine zinaongezeka zikiwemo binafsi ikiwa ni hatua itayoifanya serikali kukusanya kodi zaidi na kukuza mapato ya nchi.

Alisema katika utawala wake atafanyakazi zake na makundi yote ya kijamii wakiwemo wanawake, vijana na wazee kwa kuwawekea mazingira bora ya maisha yao wakiwemo wasanii na wanamichezo.

Alisema dhamira ya serikali ijao ni kuona inakuwa na uchumi utaoweza kumfikia kila mtu hasa vijana kuwa tayari kushiriki katika kukuza mapato yao kwa vile wananchi wa Zanzibar wanahitaji maendeleo.

“Lazima Tufungue njia za kiuchumi kwa kuwa na mazingira mazuri ya biashara huru na kodi inakusanywa ipasavyo, maana awamu zote zimefanya mazuri nitayaendeleza” alisema Dk. Hussein.

Alisema katika kuifanyakazi hiyo atahakikisha miradi ya maendeleo iliyoanzisha katika awamu hizo ataiendeleza na baada ya kukamilika mwaka ujao ataanzisha mipya.

Kuhusu kushirikiana na serikali ya Muungano, Dk. Mwinyi, alisema atahakikisha anaendeleza mahusiano mazuri, kwa vile baadhi ya mikopo na misaada ya miradi ya maendeleo huhitaji idhini ya serikali hiyo.

Akizungumzia juu ya uchaguzi Mkuu ujao, alisema anamatumaini makubwa utafanyika kwa Amani na utulivu, kwa vile serikali imejipanga kuona hli hiyo inatawala kote nchini.

Alisema Chama cha CCM kitafanya vizuri na kitafanikiwa kushika dola, kwa vile kina wanachama wengi na wananchi, wanakiunga mkono jambo ambalo halina wasiwasi wa ushindi.

Aliwataka wananchi na vyama vya siasa kuona wanafanya kampeni za kistaarabu ili uchaguzi uweze kufanyika kwa Amani na utulivu. 

Dk. Mwinyi akifafanua juu ya adhama ya kupambana na Rushwa na maovu ndani ya serikali akiingia madarakani, alisema suala hilo halina mjadala kwa sasa kwani ni maeneo makubwa atayoyapa kipau mbele.

Alisema Zanzibar ina raslimali nyingi inayohitaji kusimamiwa vyema na haiwezekani serikali ikawalinda wanaozuiya maendeleo yasiongezeke na ni lazima wadhibitiwe.