MJUMBE wa Taasisi ya Al Miraaj Dk. Hussein Ali Mwinyi amesema ataendelea kushirikiana na taasisi mbalimbali nchini ambazo zimekuwa zikisaidia wananchi.

Kauli hiyo aliitoa wakati akikabidhi msaada wa nyama iliyotolewa na taasisi hiyo kwa wananchi wasiojiweza wa Masingini wilaya ya Magharibi ‘A’ kwa ajili ya sikukuu ya Eid Hajj.

Dk. Mwinyi ambae ni mgombea wa Urais wa Zanzibar kwa tiketi ya Chama cha Mapinduzi, alisema endapo atakuwa rais wa Zanzibar basi ataendeza uhusiano huo ili waliowengi waweze kunufaika na misaada hiyo.

“Tasisi hiii imekuwa ikinisadia wakati nilipokuwa Mbunge wa Jimbo la Kwahani na hata kule bara jimbo la Mkuranga hivyo naahidi mashirikiano yetu yataendelea ili kuona wanaendelea kutoa misaada kwa wananchi wetu,” alisema. 

Aliishukuru jumuiya hiyo kutoa sadaka kwa ajili ya wananchi wa Zanzibar wasiojiweza nao waweze kusherehekea sikukuu kama watu wengine.

“Naamini waliowengi katika eneo hili watafaidika na sadaka hii kwani tasisi hii inatusaidia sana sisi kutupatia misaada mbalimbali kwa ajili ya wananchi wetu,” alisema.

Hivyo aliziomba tasisi nyengine zenye uwezo kuendelea kusaidia ili waweze kupata radhi za Mwenyezimungu.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Jumuiya hiyo Tanzania, Sheikh Arif Yussuf Abdul-rahman, alisema, lengo la msaada huo ni kusaidia wananchi mbalimbali ikiwemo mayatima, walemavu na makundi mengine.

Aidha, alisema ni kawaida ya tasisi hiyo kuchinja na kutoa misaada mbalimbali kwa ajili ya kuwasaidia watanzania wanyonge ili waweze kupata kitoweo kwa ajili ya sikukuu.

Hivyo, aliahidi kuendelea kutoa misaada hiyo katika maeneo mbalimbali ya Tanzania na kuziomba tasisi nyengine kujenga utamaduni wa kutoa misaada kwa wasiojiweza ili waweze kupata radhi za Mwenyezimungu.

Kwa upande wake Sheikh Othman Maalim aliwasisitiza waislam wenye uwezo kuchinja katika kipindi cha sikukuu ya Eid Hajj kwani ni ibada kubwa mbele ya allhah.

“Kuchinja mnyama kama kondoo, ngamia, mbuzi, ng’ombe katika kipindi hichi ni sunna na thawabu kubwa mbele ya Allah siku ya kiama hasa kuwapa masikini,” alisema.

Jumla ya ng’ombe 100, mbuzi 100 na ngamia watatu wamechinjwa kwa ajili ya sadaka katika kipindi hichi cha sikukuu ya eid Hajj.