NA KHAMISUU ABDALLAH

MGOMBEA wa urais wa Zanzibar kwa tiketi ya Chama cha Mapinduzi, Dk. Hussein Mwinyi, atawahutubia wanaCCM baada ya kuchukua fomu ya kuwania kuteuliwa nafasi hiyo toka Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC).

Katibu wa Kamati Maalum ya NEC, Idara ya Itikadi na Uenezi CCM Zanzibar, Catherine Peter Nao, alieleza hayo jana alipozungumza na waandishi wa habari huko ofisi kwake Kisiwandui mjini Zanzibar.

Alisema mgombea huyo mara baada ya kuchukua fomu toka Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC), atakwenda ofisi kuu ya CCM Kisiwandui kwa ajili ya kuzungumza na wanaCCM na wananchi.

“Tunaamini hatakosa maneno ya kutuambia kwani wakati tunampokea kutoka Dodoma alituambia yajayo yanafurahisha”, alisema katibu huyo.

Aliwataka wanaCCM na wananchi wapenda amani na maendeleo kujitokeza kwa wingi ili kumsikiliza mgombea huyo nini anataka kuwaeleza wananchi wa Zanzibar.

“Sheria inatwambia atasindikizwa na watu wasiopungua 20 na tayari viongozi wameshapangwa ambao watakwenda ZEC kwa ajili ya kumsindikiza, sisi tutakuwepo kwa ajili ya kumsubiri wakati anarudi”, alisema.

Catherine, alibainisha kuwa CCM ndio chama kilichounda serikali hivyo haitakuwa tayari kuvunja sheria na badala yake itahakikisha inafuata sheria na miongozo yote ili iwe mfano kwa vyama vyengine.

Mbali na hayo, alisema CCM ina kila sababu ya kushinda katika uchaguzi mkuu mwaka huu katika nafasi zote hasa nafasi ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Rais wa Zanzibar.

“Hatuna wasiwasi kwa Tanzania bara tutashinda kwa asilimia 95 na Zanzibar 85 kwani uwezo huo tunao kutokana na serikali za CCM zilivyotekeleza maendeleo kwa wananchi ni makubwa”, alisema.