NA MWANAJUMA ABDI, DODOMA

MGOMBEA Urais wa Zanzibar, Dk. Hussein Mwinyi amewataka wanaCCM, wapenzi wa chama hicho na wananchi kwa ujumla, kuhakikisha wanajitokeza kwa wingi Oktoba 28 mwaka huu kwenda kuwapigia kura wagombea wote wa CCM.

Dk. Mwinyi alieleza hayo jana mjini Dodoma alipopewa nafasi ya kuwasalimia wanaCCM na wananchi wa Tanzania kwenye uzinduzi wa kampeni za chama hicho kwa ajili ya uchaguzi mkuu.

Mgombea huyo wa nafasi ya urais wa Zanzibar alisema ili CCM iweze kupata ushindi wa kishindo, lazima wanachama, wapenzi na wananchi wote waliojiandikisha wahakikishe wanawapigia kura wagombea wote wa chama hicho.

Dk. Mwinyi alisema hana shaka ya ushindi wa CCM kwenye uchaguzi mkuu mwaka huu hasa ikizingatiwa kuwa imetekeleza vyema ilani ya uchaguzi, hata hivyo lazima watu wajitokeze wakipigie kura ili ushindi uwe wa kishindo.

“Hatuna shaka ya ushindi kwenye uchaguzi mkuu wa mwaka huu, hata hivyo tunataka ushindi wa kishindo ambao unatokana na wanaCCM, wapenzi, na wananchi wote kukipigia kura chama chetu”, alisema Dk. Mwinyi.

Katika hotuba hiyo, fupi Dk. Mwinyi alimshukuru rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Ali Mohamed Shein kutokana na hatua yake ya kusimamia vyema utekelezaji wa ilani ya Chama cha Mapinduzi.

Dk. Mwinyi alisema Zanzibar ya miaka 10 chini ya uongozi wa Dk. Ali Mohamed Shein imepiga hatua kubwa za kiuchumi, kimaendeleo na huduma za jamii kama afya, miundombinu ya barabara, maji na elimu.

Alieleza kwa upande wa Rais wa Tanzania, ambae ni mgombea urais wa Tanzania Dk. John Pombe Magufuli kwa miaka mitano amefanya mambo makubwa ya kimaendeleo kupitia ilani ya uchaguzi.

Hata hivyo, aliwasihi wananchi kudumisha amani ya nchi kwa lengo la kuwaletea maendeleo watanzania kwa vile bila ya amani hakuwezi kufikia hatua ya mafanikio.

Alisema vipoi viashiria vimeanza kujitokeza vya kutaka kuvuruga amani, na kuwataka wananchi wahakikishe wanajiepusha na uchafuzi wa amani.

Mapema asubuhi wanaCCM waliingia katika kiwanja cha Jamhuri wakiwa wamevalia nguo zao za kijani na manjano ambao walipendezeshwa na wasanii wa kizazi kipya na ngoma za asili waliotumbuiza uwanjani hapo.

Kwa kipindi chote wanaCCM walitulia kusikiliza sera za chama hicho na huku wabunge wa Dodoma wakiahidi kura zote zitapatikana kwa kufanya kampeni nyumba kwa nyumba, shuka kwa shuka na mtu kwa mtu.