NA ABDI SHAMNA, IKULU

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Ali Mohamed Shein amesema wizara ya Kazi, Uewezeshaji, Wazee, Wanawake na Watoto inapaswa kukaa pamoja na uongozi wa kituo cha wanawake kinachotengeneza vifaa vya umeme wa jua ‘Barefoot College’ ili kuandaa mwelekeo wa kituo hicho.

Dk. Shein alisema hayo jana huko Kinyasini katika sherehe za kutimiza miaka mitano tangu kuanzishwa kwa kituo hicho, hafla iliyokwenda sambamba na ufunguzi wa jengo jipya la dahalia kwa ajili ya wanafunzi 

Alisema kwa kuzingatia sera na maelekezo ya serikali, wizara hiyo inapaswa kukaa pamoja na uongozi wa kituo hicho na kuanza kufikiria mahitaji ya baadae ya kituo, ikiwemo eneo la ardhi litakalotumika kwa ajili kuongeza majengo na baadhi ya nyenzo muhimu zitakazohitajika.

Alisema kuwepo kwa changamoto mbali mbali, ikiwemo uhaba wa madarasa na mabara ya kufundishia, ukosefu wa mahala pa kusalia kwa ajili ya washiriki wengi wa mafunzo na ukosefu wa lami katika eneo dogo la barabara inayoingia kituoni hapo ni mambo yanayohitaji kutafutiwa ufumbuzi.

Alisema kuna umuhimu wa kukiendeleza kituo hicho kwa kuzingatia hali halisi ya mazingira ya Zanzibar na mabadiliko ya dunia.

Dk. Shein aliuagiza uongozi wa kituo hicho kuunda jumuiya ya wanafunzi wanaomaliza mafunzo kituoni hapo pamoja na kutoa mialiko ya kufika kituoni ili kueleza namna walivyofaidika na mafunzo, jinsi wanavyoitumia taaluma waliyoipata.

Alieleza kuwa kuna mafanikio makubwa yaliopatikana na kituo hicho ndani ya kipindi cha miaka mitano na kuwashukuru waliochangia katika kufanikisha uendeshaji wa kituo hicho.

Alisema ni jambo la kujivunia kuona kituo hicho kinapokea wanafunzi kutoka Tanzania bara na nchi za jirani na kubainisha kuwa hilo ndio lengo la serikali tangu kituo hicho kilipoanzishwa.

Aliipongeza serikali ya India kwa kuendelea kuunga mkono juhudi za Zanzibar katika kukiendeleza kituo hicho na kwamba ufunguzi wa jengo hilo ni uthibitisho wa ushirikiano baina ya nchi hizo.

Alisema serikali na jumuiya ya Umoja wa Ulaya zimeshrikiana kufanya tafiti juu ya uwezekano wa kupata nishati hiyo, huku matokeo yakionesha kuwepo uwezekano mkubwa wa kupata kiwango kikubwa cha umeme kupitia chanzo cha jua.

Aidha, Dk. Shein alibainisha juhudi mbali mbali zinazochukuliwa na serikali katika kuwawezesha na kuimarisha ustawi wa wanawake, kupitia Mfuko wa Uwezeshaji wananchi kiuchumi pamoja na ule wa Vijana unaotekelezwa na  Serikali kwa kushirikiana na Uongozi wa Mfuko wa Khalifa Fund.

Katika hafla hiyo Dk. Shein alipata fursa ya kutembelea na kuangalia kazi za ujasiriamali zinazoendeshwa na washriki wa mafunzo ya kituo hicho pamoja na kupokea zawadi mbali mbali kwa ajili yake na Mama Mwanamwema Shein.

Mapema, Waziri wa Kazi, Uwezeshaji, Wazee, Wanawake na watoto, Moudline Castico, alisema wizara hiyo itaendelea na juhudi za kukiendeleza kituo hicho ili kufanikisha dhamira ya kuanzishwa kwake.

Nae, Balozi Mdogo wa India nchini, Bhagwant Singh alisema Serikali ya India itaendelea kuunga mkono juhudi za kukiimarisha kituo hicho ili kuweza kupata mafanikio makubwa.

Alisema ana matumaini makubwa kuwa ushirikiano uliopo kati ya India na na Zanzibar na Tanzania kwa ujumla utaendelea kuimarika kwa maslahi ya watu wa nchi mbili hizo.

Katibu Mkuu Wizara ya Kazi, Uwezeshaji, Wazee, wanawake na watoto Fatma Gharib Bilali alisema jumla ya akinamama 45 wamenufaika kutokana na mafunzo ya utengenezaji wa vifaa vya umeme wa jua.

Alisema jumla ya nyumba 958 kutoka shehiya mbali mbali za Unguja na Pemba tayari zimeunganishwa umeme wa jua kupitia washiriki wa mafunzo ya kituo hicho.

Mkuu wa kituo cha Barefoot College, Pendo alisema pamoja na mafanikio makubwa yaliopatikana katika uendeshaji wa kituo hicho, kuchelewa kupatikana vifaa vya umeme wa jua ni miongoni mwa changamoto zinazokikabili kituo hicho.

Kituo cha Barefoot College, kilizinduliwa rasmi na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein mnamo Augosti 6, 2015.