Asema: Serikali imekiwekea mikakati kilimo

Bajeti yaongezwa, hakuna upungufu wa chakula

KHAMISUU ABDALLAH NA LAILA KEIS

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Ali Mohamed Shein amesema serikali kwa kuzingatia umuhimu wa chakula na lishe inaendelea kutekeleza kwa vitendo sheria namba 5 ya mwaka 2011, ambayo inatoa uhakika wa kuwepo kwa chakula nchini.

Dk. Shein aliyasema hayo wakati akifungua maonesho ya tatu ya wakulima ya nane nane katika viwanja vya Dole, ambapo alisema lengo la sheria hiyo ni kuandaa mazingira yatakayoiwezesha Zanzibar kwa wakati wote kuwa na chakula cha kutosha, lishe iliyokuwa bora.

Alisema, mikakati mengine ni mpango wa maendeleo wa miaka 10 wa sekta ya kilimo, mpango wa maendeleo ya uvuvi na mkakati wa mazao ya baharini.

Dk. Shein alibainisha kwamba mikakati hiyo imelenga kuongeza uzalishaji kwa kutumia mbinu bora, teknolojia za kisasa, ujenzi wa miundombinu, upatikanaji wa masoko, upatikanaji wa mitaji na uhifadhi wa chakula ili kuongeza tija, kipato, kuondoa umasikini na kukuza uchumi wa nchi.

Alisema katika kuimarisha sekta hiyo kwa mwaka wa fedha 2020/2021 serikali imeongeza bajeti kutoka shilingi bilioni 88.17 hadi 2019/2020 hadi kufikia bilioni 129.89 kwa mwaka 2020/2021 ambapo ongezeko hilo ni sawa na asilimia 47.3.     

Alisema maonesho ya nane nane ni mbinu bora iliyobuniwa na serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na imeleta mafanikio makubwa ya wakulima nchini na taifa kwa ujumla.

Alibainisha kuwa maonesho hayo yamebuniwa kwa makusudi na mambo mbalimbali ikiwemo kuwatia hamasa wananchi kutumia vizuri rasilimali ya ardhi katika shughuli zenye faida kwao kwa lengo la kupata tija ya kupitia sekta hiyo.

Alisema jambo jengine ni kuwashajihisha wakulima kuongeza bidii katika kuimarisha bidhaa ili ziweze kuwa na ubora unaohitajika sambamba na kuwajumuisha na kuwashajihisha wananchi ili wapate fursa ya utaalamu na njia ya kuimarisha ubora wa bidhaa.

Sambamba na hayo alisema malengo mengine ya serikali ni kuwawezesha wakulima kupata soko la bidhaa zao na kuwaunganisha na masoko mengine na watoa huduma muhimu kwa lengo la kuwanasua katika hali ya umasikini.

“Lengo la serikali yenu ni kuona mnaondokana na utegemezi na unyonge wa kipato pamoja na kuisaidia nchi yenu kupunguza gharama za uagizaji bidhaa kutoka nje ya nchi”, alisema.

Mbali na hayo Dk. Shein, alisema maonesho hayo ni mbinu moja ya kufikia malengo hayo ambayo hatua mbalimbali zimeanza kuchukuliwa, hivyo ni vyema wakulima kuongeza nguvu ari na kasi ya kuona na Zanzibar inafanikiwa kama nchi nyengine.

Alisema kujitegemea kwa chakula ni jambo la msingi kwani wakati dunia ilipokumbwa na maradhi ya corona Tanzania ikiwemo Zanzibar ilikuwa na chakula cha kutosha jambo ambalo liliondosha hofu miongoni mwa wananchi.

Alisema maradhi hayo ni fundisho kubwa katika kuendeleza na kuimarisha shughuli za kilimo, mifugo na uvuvi ili ziweze kusaidia katika mahitaji ya kila siku na pale inapotokezea maafa ya dunia.

Alisema shughuli za kilimo na uvuvi ni miongoni mwa mambo ya urithi ulioachwa tokea kale na dahari hivyo sio vyema mtu kudharau vya kwao na badala yake wana kila sababu ya kuendeleza kazi zao za asili.

Aliwapongeza washiriki wa maonesho hayo kwa kuunga mkono juhudi za serikali katika kuifanikisha mipango yake ya maendeleo kama ilivyoainishwa ikiwemo Mkuza 111, dira ya maendeleo ya 2020 na ilani ya CCM ya uchaguzi ya mwaka 2015/2020 ambazo zinamaliza muda.

Alisema utekelezaji wa mikakati hiyo inakwenda sambamba na tafsiri ya malengo endelevu ya milenia ya ajenda ya 2030 ambayo lengo namba mbili ya ajenda hiyo ni kuwa na uhakika wa chakula, lishe bora na kilimo endelevu kwa madhumuni ya kumaliza njaa ulimwenguni.

Kwa upande wake Kaimu Waziri wa Wizara ya Kilimo Maliasili Mifungo na Uvuvi, Haji Omar Kheir, alipongeza hatua ya serikali ya awamu ya saba kwa kuiendeleza sekta ya kilimo.

Aliahidi wizara itaendeleza maonesho hayo ili kuona wakulima wanapata fursa ya kutangaza na kuimarisha kilimo chao kwa maslahi yao na taifa kwa ujumla.    

Kwa upande wake Katibu Mkuu wa wizara hiyo, Maryam Juma Sadala, alisema maonesho hayo yamejumuisha taasisi 219 kwa mwaka huu ukilinganisha na mwaka jana walikuwa 172 ambayo ni hatua maendeleo makubwa ambayo yameonesha ari na muamko kwa wadau mbalimbali wa sekta hiyo.

Hata hivyo, alisema wamefanya jambo la busara kuanzisha maonesho hayo ambayo yanawaunganisha wakulima, wafugaji wavuvi na wahifadhi mazingira katika kutoa huduma na kupata fursa ya kuona maendeleo ya sekta hiyo hapa nchini.

Alisema maonesho hayo yanaunganisha watu mbalimbali kwa kutoa huduma na kuunganisha fursa zilizokuwepo ili waweze kupiga hatua katika kupambana na umasikini na kupiga hatua katika uchumi wa nchi.

Maonesho hayo yamegharimu zaidi ya shilingi milioni 71 ambazo zinatoka serikalini na zaidi ya shilingi milioni 12 zimechangiwa na washiriki na wajasiriamali ambapo kauli mbiu ya mwaka huu ya nane nane ni ‘Tudumishe amani na utulivu kwa maendeleo ya sekta ya kilimo Zanzibar’.