NA RAJAB MKASABA, IKULU
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Ali Mohamed Shein ameutaka uongozi wa wizara ya Katiba na Sheria kuyatuamia mafanikio yaliyopatikana kwenye awamu ya saba ili yaweze kuwa kichocheo cha mafanikio katika wamu ijayo.
Dk. Shein alieleza hayo jana ikulu jijini Zanzibar alipokutana na uongozi wa wizara hiyo wakati ilipowasilisha taarifa ya utekelezaji wa mpango kazi wa mwaka 2019/2020 na mpango kazi wa mwaka 2020/2021.
Katika kikao hicho, Dk. Shein aliwasisitiza viongozi wa wizara hiyo kuongeza kasi kwani sekta ya sheria imepata mafanikio makubwa yanafanana na yale yanayopatikana katika nchi nyengine zilizoendelea.
Alisema serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imeweka mazingira mazuri katika sekta ya sheria, hivyo ni vyema sekta hiyo ikaendelea kuwatumikia wananchi.
Dk. Shein alifahamisha kuwa awamu za uongozi katika serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar zimefuata sheria na katiba zilizopo na kwamba pale inapotokea umuhimu wa kufanywa marekebisho hufanywa kwa maslahi ya nchi na wananchi.
Alielezea furaha yake kwa uongozi wa wizara hiyo na kupokea shukurani na pongezi kutoka kwa uongozi huo ambazo zimetolewa kwa niaba na Naibu Kadhi Mkuu wa Zanzibar, Sheikh Othman Ngwali.
Alisema kuwa sekta ya sheria imefanya kazi kubwa hapa nchini kwa kuchangia katika kuifikisha Zanzibar kuwa na Uchumi wa Kati kwani bila ya Sheria mafanikio hayo yasingelifikiwa hasa ikizingatiwa kwamba uchumi unakwenda sambamba na Utawala Bora.
Nae Katibu Mkuu Kiongozi na Katibu wa Baraza la Mapinduzi Dk. Abdulhamid Yahya Mzee alisema kuwa mikutano hiyo ya (Bango Kitita) ina msaada mkubwa katika wizara za serikali na kueleza haja ya kuendelezwa.
Mapema Waziri wa Wizara ya Katiba na Sheria, Khamis Juma Mwalim alitoa pongezi kwa Dk. Shein kwa kuwaongoza vyema katika utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) ambapo Wizara hiyo inajivunia kutekeleza kwa mafanikio makubwa Ibara ya 121 (d) na (e).
Alisema uimarishaji wa taasisi za sheria umepata msukumo mkubwa katika kipindi cha uongozi wa Dk. Shein kwa kuzitekeleza shughuli kadhaa zikiwemo za kufanyia mapitio sheria zilizopitwa na wakati, ujenzi wa mejengo ya mahakama na kuongeza idadi ya majaji.
Alieleza kuwa kazi iloyofanywa na Tume ya kurekebisha Sheria ya kuzifanyia mapitio Sheria 22 kati ya Sheria 37 zimekamilika na kuwasilishwa katika Mamlaka husika ambapo kasi hiyo imechangia kuzifanyia mapitio sheria nane zinazohusu masuala ya ardhi ambapo ikikamilika itapelekea kupunguza kwa kiasi kikubwa migogoro ya ardhi na kuweka utaratibu bora wa matumizi na usimamizi wa ardhi.
Pia, Waziri huyo alieleza mambo mbali mbali yaliyotekelezwa na Wizara hiyo ikiwa ni pamoja na kuandaa Sheria mbali mbali ikiwemo Sheria ya Jumuiya ya Mawakili Zanzibar, Sheria ya Mawakili, Sheria ya Mufti na Sheria ya Skuli ya Sheria.
Aidha, alieleza kuwa ujenzi wa jengo la Mahakama Kuu Tunguu unaendelea vizuri ambapo hadi kufikia tarehe 30 Juni 2020 utekelezaji halisi ulifikia asilimia 55 wakati makadirio yake ni kufikia asilimia 65 ya ujenzi wote.
Waziri Mwalimu alieleza kuwa uratibu wa masuala ya kidini umeendelea ambapo Kamisheni ya Wakfu na Mali ya Amana imeendelea na hatua za kuanzisha mfuko wa Hijja ambapo matarajio ni kuuzindua katika mwaka huu wa fedha.
Uongozi huo ulieleza kuwa sekta ya Sheria imeimarika na Wanasheria wamekuwa na hadhi kubwa sana ikilinganisha na miaka ya nyuma ikiwa ni pamoja na kutungwa Sheria na kuwepo kwa Chuo cha Sheria cha kwenda kujifunza ambapo yote hayo yamepatikana katika uongozi wake.
Wakati huo huo, Dk. Shein alikutana na uongozi wa Wizara ya Kazi, Uwezeshaji Wazee, Wanawake na Watoto na kuusisitiza uongozi huo kuendeleza mashirikiano, nidhamu, heshima, kupendana sambamba na kujenga udugu katika sehemu za kazi.
Nae Waziri wa Wizara hiyo Maudline Cyrus Castico alieleza kuwa kuanzishwa kwa Wizara hiyo ni kithibitisho cha namna anavyoumwa na maendeleo ya wananchi wake na kutekeleza Sera za Kitaifa na Kimataifa za kutaka mtu yoyote asiachwe nyuma katika kupata fursa za kimaendeleo.
Alisema kuwa Dira ya Wizara hiyo ni kuwa na jamii ya Wazanzibari yenye Ajira za Staha, ubunifu na uwezo wa kukabiliana na umasikini, inayotoa haki na fursa sawa kwa watu wa makundi yote huku uongozi ukipongeza kupata ofisi nzuri Unguja na Pemba sambamba na kuifanya Pencheni ya Wazee kuwa ni Sheria.
Aidha, ungozi huo ulimpongeza Mke wa Rais wa Zanzibar Mama Mwanamwema Shein kwa kuiunga mkono Wizara hiyo sambamba na kuwa nao pamoja viongozi wake.
Pia, Dk. Shein alikutana na uongozi wa Wizara ya Kilimo, Maliasili, Mifugo na Uvuvi chini wa Waziri wake Mmanga Mjengo Mjawiri ambapo alieleza kuwa Wizara hiyo imelenga kuendeleza mageuzi katika sekta ya kilimo kwa kukifanya kilimo cha kisasa, jumuishi na chenye ushindani ambacho kinachangia katika sekta ya viwanda na utalii ili kuleta tija na maisha bora ya wananchi wa Zanzibar na maendleo ya uchumi kwa jumla.
Alisema kuwa sekta ya kilimo ikijumuisha mazao, mifugo, uvui, misitu na rasilimali zisizorejesheka bado inaendelea kuwa ni muhimili mkuu wa uchumi wa Zanzibar.
Aliongeza kuwa sekta hiyo inatoa mchango wa moja kwa moja kwa wananchi katika kujikimu kimaisha ambapo asilimia 40 wameajiriwa na sekta hiyo na inakadiriwa kwua Zaidi ya asilimia 70 ya wananchi wanategemea sekta hiyo ambapo kwa mwaka 2019 imechangia asilimia 21.2 ya Pato la Taifa.
Akieleza kuhusu wizi na uchimbaji holela wa rasilimali ya mchanga, Waziri huyo alisema kuwa Wizara kwa kushirikiana na vikosi vya SMZ imeunda kikosi shirikishi cha doria ambacho kinaendelea kupambana na wizi na uchimbaji wa mchanga kiholela pamoja na udhibiti wa ukataji ovyo wa miti.