Aagiza kasi utekelezaji majukumu

NA ABDI SHAMNA, IKULU

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Ali Mohamed Shein ameuagiza uongozi wizara ya Vijana, Utamaduni, Sanaa na Michezo kuongeza kasi ya uwajibikaji katika kuelekea uchaguzi mkuu.

Dk. Shein alieleza hayo jana ikulu mjini Zanzibar, alipokutana na uongozi wa hiyo wakati ilipowasilisha taarifa ya utekelezaji wa mpango kazi wa mwaka 2019/2020 na mpango kazi wa mwaka 2020/2021.

Alisema kuna umuhimu kwa uongozi wa wizara hiyo kuongeza kasi katika usimamizi na uwajibikaji wa majukumu ya kazi kwa kuzingatia shughuli za serikali zinapaswa kuendelezwa kama kawaida hadi pale awamu ijayo itakapochukua nafasi yake.

Dk. Shein alisema Zanzibar inahitaji kuwa na uwanja mkubwa wa kisasa utakaowezesha kufanyika shughuli mbali mbali za kitaifa.

Alisema kuna umuhimu wa kuwa na uwanja wa aina hiyo, utakaokuwa na uwezo wa kufanyika matukio ya kitaifa, kama vile gwaride na michezo ya aina tofauti, ikiwemo mpira wa miguu.

Alisema uwanja wa Amani hauwezi kukidhi mahitaji ya wakati na hivyo akautaka uongozi wa wizara hiyo kuangalia maeneo ya nje ya mji, likiwemo eneo la Tunguu.

Katika hatua nyengine, Dk. Shein alipokea salamu na kuupongeza uongozi wa wizara hiyo kwa hatua yake ya kuwatembelea wasanii wakongwe na walioiletea sifa kubwa Zanzibar.

Alisema utaratibu wa kuwatembelea wasanii hao ni jambo jema na linalopasa kuendelezwa na kufanyika mara mbili kwa mwaka ikiwa ni hatua ya kuunga mkono na kuthamini juhudi walizofanya, sambamba na kukubali wazo la kuanzisha mfuko wa kuwasaidia wasanii wa aina hiyo.