Ajivunia mafanikio kiuchumi, kijamii 

NA ABDI SHAMNA, IKULU

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Ali Mohamed Shein amesema Zanzibar imepata mafanikio makubwa ya kiuchumi na kijamii kutokana na jitihada za vIongozi na wananchi.

Dk. Shein alisema hayo huko ikulu jijini Zanzibar, alipokutana na uongozi wa Ofisi ya Rais, Utumishi wa Umma na Utawala Bora ilipowasilisha taarifa ya utekelezaji wa mpango kazi kwa mwaka 2019/2020 na mpango kazi wa mwaka 2020/2021.

Alisema maendeleo ya kiuchumi yaliyofikiwa katika sekta mbali mbali, ikiwemo miundombinu na usafirishaji, upandishaji wa mishahara mara tano, ongezeko la pencheni na mambo mengine kadhaa yanatokana na juhudi za serikali.

Dk. Shein aliutaka uongozi wa Ofisi hiyo kuandaa utaratibu wa mipango ya mafunzo kwa watumishi wa serikali kwa kuzingatia mahitaji ya wizara husika na serikali kwa ujumla na kubainisha kuwa hiyo ndio kazi ya utumishi wa umma.  

Aidha, aliuagiza uongozi wa ofisi hiyo kuweka kumbukumbu za muhtasari wa ongezeko la mshahara na ulipaji wa posho katika mashirika ya serikali na kusisitiza wajibu wa waziri kuwa ndiYe mwenye mamlaka ya kuidhinisha kiwango cha malipo baada ya kupendekezwa na bodi. 

Alisema pamoja na mipango ya chuo Cha Utumishi wa Umma kuwa na azma ya kuendesha mafunzo ya uongozi, kinapaswa kuwa na mwelekeo wa mbali zaidi utakaolenga kukiimarisha na kukifanyia utanuzi.

Dk. Shein aliupongeza uongozi, watendaji na wafanyakazi wa wizara hiyo kwa utekelezaji mwema wa majukumu ya kazi zao na maandalizi na uwasilishaji mzuri wa taarifa ya utekelezaji wa mpango kazi.

Kwa upande wake, Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Balozi Seif Ali Iddi alisema mafanikio yaliyopatikana na Ofisi hiyo, kutokana na kuwepo kwa uongozi bora.

Aliitaka Mamlaka ya Kuzuia Rushwa na Kuhujumu uchumi Zanzibar (ZAECA) kuendelea kufanya kazi zake kwa umakini na weledi mkubwa ili kukabiliana na tatizo la rushwa.

Naye, Katibu Mkuu wa Baraza la Mapinduzi na Katibu Mkuu Kiongozi, Dk. Abdulhamid Yahya Mzee aliwapongeza viongozi, watendaji na wafanyakazi wa ofisi hiyo kwa mashirikiano yao yaliyowawezesha kutekeleza vyema majukumu yao.