NA RAJAB MKASABA, IKULU
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Ali Mohamed Shein jana aliongoza mazishi ya mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi, wilaya ya Amani Kichama marehemu Juma Khamis Haji (Juma Resi), yaliyofanyika kijijini kwao Upenja.
Katika mazishi hayo viongozi mbalimbali wa vyama vya siasa na serikali, walihudhuria ikiwa pamoja na wananchi, ndugu na jamaa.
Miongoni mwa viongozi wengine waliohudhuria ni pamoja na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Balozi Seif Ali Iddi, Naibu Katibu wa CCM Zanzibar Abdallah Juma Mabodi na Naibu Kadhi Mkuu wa Zanzibar, Sheikh Hassan Othman Ngwali.
Awali Dk. Shein aliungana na viongozi, ndugu, jamaa, marafiki na wananchi mbali mbali katika swala ya jeneza iliyofanyika katika msikiti wa Upenja, wilaya ya Kaskazini ‘B’.
Katika uhai wake Juma Khamis Haji (Juma Resi), aliyezaliwa mwaka 1951 amekitumikia Chama cha Mapinduzi (CCM) katika nyadhifa mbali mbali ikiwa ni pamoja na kuwa Diwani wa Jimbo la Mwembemakumbi, Katibu wa jimbo la Mwembemakumbi, Mwalimu wa madarasa ya itikadi pamoja na makundi ya vijana wa hamasa.
Nafasi nyengine ni ofisa uhamasishaji wilaya, mjumbe wa mkutano mkuu wa CCM Taifa na mjumbe wa mkutano mkuu wa Mkoa, katibu mwenezi wilaya ya mjini, katibu mwenezi wilaya ya Amani, mjumbe wa halmashauri kuu ya taifa ya CCM, Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Amani Kichama, cheo ambacho alikitumikia mpaka mauti yalipomfika.
Wakati huo huo, mara baada ya mazishi, Dk. Shein alikutana na familia ya marehemu Juma Resi hapo hapo kijijini kwao Upenja na kutoa mkono wa pole kwa familia na wafiwa na kumuomba Mwenyezi Mungu awape subira katika kipindi hiki kigumu cha msiba huku akisisitiza kuendelea kumuombea dua marehemu.
Marehemu Juma Resi ameacha vizuka wawili pamoja na watoto 12 na wajukuu 23, Mwenyezi Mungu ailaze roho ya marehemu mahala pema peponi, Amin.