NA ABDI SHAMNA, IKULU

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Ali Mohamed Shein ameupongeza uongozi na watendaji wa wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali kwa kazi nzuri waliyofanya katika kipindi cha miaka 10 ya uongozi wake.

Dk. Shein alitowa pongezi hizo ikulu jijini Zanzibar, alipokutana na uongozi wa wizara hiyo wakati ilipowasilisha taarifa ya utekelezaji ya mpango kazi kwa mwaka 2019/2020 na mpango kazi wa mwaka 2020/2021.

Alisema wizara hiyo yenye idara na taasisi kadhaa zinazotegemeana imepata mafanikio makubwa katika kuimarisha sekta ya elimu nchini.

Dk. Shein aliwataka viongozi na watendaji wa wizara hiyo kuendeleza juhudi zilizofanikisha mafanikio hayo na kubainisha kuwa zimeleta sifa na manufaa makubwa kwa taifa na wananchi wake.

Aliutaka uongozi wa wizara hiyo kufikiria njia ya kupata fedha kupitia mashirika ya kimataifa kama vile benki ya Dunia na ADB ili kuweza kuanzisha jengo jipya na la kisasa kwa ajili ya huduma za maktaba litakaloweza kukidhi mahitaji ya wakati.

Aliutaka uongozi wa wizara hiyo kuwatumia wana taaluma wazalendo waliobobea katika masuala mbalimbali ya kielimu yanayohitaji ushauri, badala ya kazi za namna hiyo kuzitangaza kwa wataalamu kutoka nje ya nchi.

Dk. Shein alitaka kufanyika juhudi za kuifanyia matengenezo skuli ya Mkunazini kwa kufuata miongozo ya Mamlaka ya Mji Mkongwe, ili kuepuka athari zitakazojitokeza za kuanguka kwa jengo hilo na kuleta maafa.

NaYe, Makamu wa Pili wa Rais, Balozi Seif Ali iddi, alisema kumekuwepo maktaba za aina mbali mbali, hivyo akautaka uongozi wa Idara ya Huduma za Maktaba kufanya juhudi za kuwahamasisha wananchi na wanafunzi kutumia maktaba ziliZopo ili kupanua wigo wa uwelewa.

Naye Katibu Mkuu wa Baraza la Mapinduzi na Katibu Mkuu Kiongozi, Dk. Abdulhamid Yahya Mzee aliipongeza wizara hiyo kwa hatua kubwa za maendeleo zilizofikiwa, na kuutaka uongozi wa Wizara hiyo kuyalinda na kuyaendeleza mafanikio hayo.

Vile vile aliutaka uongozi wa wizara hiyo kusimamia utendaji wa kazi kwa watumishi katika kipindi hiki cha kuelekea uchaguzi mkuu, sambamba na kuondokana na matumizi mabaya ya mali na rasilimali za serikali, ikiwemo uuzaji wa mali zake, hususan magari.

Awali waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali, Riziki Pembe Juma, alisema katika kipindi hicho wizara hiyo imepata mafanikio makubwa ya kuimarisha sekta ya Elimu, hatua iliyotokana na juhudi kubwa za Serikali ya Awamu ya saba, chini ya uongozi wa Dk. Ali Mohamed Shein.

Aliyataja baadhi ya mafanikio hayo kuwa ni pamoja na ongezeko la ufaulu wa watahiniwa katika mitihani ya Taifa ya Kidato cha nne (F.IV) mwaka 2019 kwa daraja la kwanza, la pili na daraja la tatu.

Alisema ufaulu kwa watahiniwa wa daraja la kwanza uliongezeka kutoka watahiniwa 185 mwaka 2018 hadi watahiniwa 299 mwaka 2019, huku ufaulu wa watahiniwa wa daraja la pili ukiongezeka kutoka 903 (2018) hadi watahiniwa 1,509 (2019).

Alisema wizara hiyo ilifanikiwa kuajiri walimu 665, wakiwemo walimu 216 wa Sayansi, mwalimu mmoja wa masomo ya Ufundi pamoja na walimu 448 wa masomo ya Sanaa na Mkutubi.

Wakati huo huo, Dk. Shein alikutana na uongozi wa wizara ya Ujenzi, Mawasiliano na Usafirishaji aliipongeza wizara hiyo kwa juhudi kubwa za kuleta maendeleo.

Aliutaka uongozi wa wizara hiyo kushikana na watendaji wake na kuhakikisha ujenzi wa barabara ya Ole – Kengeja na ule wa terminal III inakamilika kabla ya uongozi wa awamu ya saba haujamaliza muda wake.

Alisema hatua hiyo itachochea ujio wa mashirika makubwa ya ndege duniani na hivyo kuimarisha uchumi wa Taifa.

Alisema masuala yote yanayoamuliwa na Bodi mbali mbali ni lazima yawasilishwe kwa Waziri anaehusika kwa ushauri kabla ya utekelezaji wake kuanza.

Naye, Waziri wa Ujenzi, Mawasiliano na Usafirishaji, Dr. Sira Ubwa Mamboya alisema katika kipindi hicho Wizara hiyo kupitia Programu ya Miundombinu na Huduma za Usafirishaji imepata mafanikio makubwa ikiwemo kukamilisha ujenzi wa barabara mbali mbali Unguja na Pemba kwa kiwango cha Lami kwa urefu wa kilomita 63.6.

Alizitaja barabara hizo kuwa ni pamoja na Bububu-Mahonda – Mkokotoni kilomita 31, Pale – Kiongele km (4.6), Matemwe – Muyuni (km 7.6), Koani – Jumbi (km 3.2), Ole – Kengeja (km 13) pamoja na barabara ya Donge – Muwanda kilomita 4.2.