NA RAJAB MKASABA, IKULU

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Ali Mohamed Shein amemtumia salamu za pongezi kwa rais wa Jamhuri ya Watu wa India, Shri Ram Kovind kwa kuadhimisha miaka 74 tangu taifa hilo lilipojipatia uhuru.

Salamu hizo zimeeleza kuwa wananchi wa Zanzibar wanaungana na ndugu zao wa India katika kusherehekea sikukuu ya uhuru wa Taifa hilo ambayo ni ya kihistoria.

Katika salamu hizo, Dk. Shein alimuhakikishia rais Ram Nath Kovind kuwa serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar itaendeleza uhusiano wa kihistoria uliopo kati yake na India sambamba na kuvumbua maeneo mapya ya mashirikiano kwa maslahi ya pande zote mbili.

Dk. Shein alimtakia kiongozi huyo na familia yake na wananchi wote wa India afya njema na sherehe njema katika kuadhimisha siku hiyo na kumtakia mafanikio zaidi ya kiuchumi kwa madhumuni ya kulinufaisha Taifa hilo na wananchi wake.

Jamhuri ya India inasherehekea siku ya uhuru wake kila ifikapo Agosti 15 ya kila mwaka ambapo nchi hiyo ilipata uhuru wake kutoka kwa Uingereza mnamo mwaka 1947 chini ya uongozi wa hayati Mahatma Gandhi.

Wakati huo huo, Dk. Shein alimtumia salamu za pongezi rais wa Jamhuri ya Watu wa Indonesia, Joko Widodo kwa kuadhimisha miaka 75 ya uhuru wa taifa hilo.

Salamu hizo za Dk. Shein alieleza kuwa uhusiano uliopo kati ya Zanzibar na Indonesia umekuwa ukiimarika kila siku na kusisitiza kuwa Zanzibar itaendeleza uhusiano na ushirikiano huo kwa ajili ya kuimarisha uchumi sambamba na kupambana na changamoto zilizopo.

“Bado kumekuwa na mahusiano mazuri kati ya serikali zetu na watu wake ambao nao wamekuwa na mashirikiano na mahusiano mema kwa ajili ya kujiletea maendeleo hatua ambayo pia, imesaidia kuleta mafanikio”, alisisitiza Dk. Shein.

Pamoja na hayo, Dk. Shein alimtakia kiongozi huyo sherehe njema na mafanikio katika kuadhimisha siku hii adhimu ya uhuru wa taifa hilo huku akimtakia afya njema, maisha marefu yeye, familia pamoja na wananchi wake sambamba na kumtakia maendeleo endelevu ya uchumi katika taifa lake.

Jamhuri ya Indonesia inasherehekea siku ya uhuru wa taifa hilo kila ifikapo Agosti 17 ya kila mwaka ambapo nchi hiyo ilipata uhuru wake kutoka kwa Uholanzi mnamo mwaka 1945 chini ya uongozi wa Sukarno Raden Sukami Sosrodihardjo.