Asema akichaguliwa Z’bar iko kwenye mikono salama

NA SAIDA ISSA, DODOMA

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Ali Mohamed Shein amewataka wanaCCM visiwani Zanzibar kumchagua mgombea wa chama hicho, Dk. Hussein Mwinyi kwani anatosha na ana vigezo vyote kuwa rais Zanzibar.

Dk. Shein alieleza hayo jana katika uwanja wa Jamhuri mjini Dodoma alipozungumza kwenye hafla ya uzinduzi wa kampenzi za Chama cha Mapinduzi kwa ajili ya uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba 28 mwaka huu.

Dk. Shein alisema ili maendeleo yaliyofikiwa Zanzibar yaendelee kustawi na kuimarishwa zaidi, lazima wananchi wa Zanzibar wamchague Dk. Mwinyi kuwa rais wa serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar wa awamu ya nane.

“Ndugu zangu Dk. Mwinyi anatosha sana, kijana huyu ni mchapa kazi na mpenda maendeleo niwaombe mumchague kwa kura nyingi za ndio ili aweze kuipeperusha bendera ya Zanzibar”, alisema Dk. Shein.

Dk. Shein ambaye pia ni makamu Mwenyekiti wa CCM Zanzibar, alisema Dk. Mwinyi ana sifa zinazotosha kuwa rais ikiwemo uzalendo wake, mpenda maendeleo na ni mchapakazi, hivyo akichaguliwa Zanzibar itakuwa kwenye mikono salama.

Katika hafla hiyo, Dk. Shein aliwaombea kura kwa upande wa Zanzibar, mgombea wa Urais wa Jamhuri ya Muungano, Dk. John Magufuli na Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan.

“Kumchagua Rais na Makamu pekee haitoshi ni lazima tuhakikishe tunachagua na viongozi wa ngazi za chini ikiwa ni pamoja na wabunge na madiwani kutoka CCM ili wakafanye kazi nzuri tena kwa ushirikiano”, alisema.

Kwa upande wake, katibu mkuu wa CCM Dk. Bashiru Ally amesema miongoni mwa maudhui mafupi ya ilani ya Chama cha Mapinduzi ni kuhakikisha inazisimamia serikali zake katika kuhakikisha kuwa zinazingatia kulinda na kudumisha misingi hiyo.

Alisema chama hicho kinaamini kwamba uzalendo kwa nchi ndio msingi wa maendeleo ya kweli ya Tanzania ambayo yataletwa na watanzania wenyewe.

“CCM itaendelea kuhimiza wananchi kuwa wazalendo kwa nchi yetu kwa kufanya kazi kwa uadilifu, bidii na maarifa kama msingi imara wa maendeleo”, alisema Dk. Bashiru.

Dk. Bashiru alisema kuwa Chama cha Mapinduzi kimepokea jumla ya shilingi Milioni 110 kutoka kwa wanaCCM na wenye mapenzi ya dhati na chama ili kuweza kusaidia katika kampeni hiyo.