NA RAJAB MKASABA, IKULU
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Ali Mohamed Shein, ameutaka uongozi wa Mkoa wa Mijini Magharibi na manispaa zake kuhakikisha mji wa Zanzibar unakua safi kwa sababu unahadhi ya jiji.
Hayo aliyasema jana ikulu alipokutana na uongozi wa Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa, Serikali za Mitaa na Idara Maalum za SMZ, wakati ilipowasilisha taarifa ya utekelezaji wa mpango kazi wa mwaka 2019/2020 na mpango kazi wa mwaka 2020/2021 ambapo Makamu wa Pili wa Rais, Balozi Seif Ali Iddi alihudhuria.
Alisema kuna haja ya kuweka mikakati kuhakikisha mji wa Zanzibar unaendelea kuvutia na kufikia malengo ya kuufanya kuwa jiji kutokana na sifa ulizonazo.
Alisema ipo haja kwa uongozi wa mkoa kuangalia suala la usafi hasa katika masoko na barabarani kwani wengi ya wafanyabiashara wamevamia maeneo hayo na hatimae kuufanya mji kutokua msafi na kuepuka ajali ambazo zinaweza kutokea.
Alieleza haja ya uongozi wa mkoa huo kuchukua hatua kwa mujibu wa sheria na taratibu zilizopo katika kuhakikisha biashara zote zinafaywa kwa kufuata taratibu na sheria zilizopo.
Alieleza kuwa licha ya serikali kubuni mpango wa masoko mapya, hata hivyo katika eneo la soko la Mwanakwerekwe bado kuna msongamano wa wafanyabishara ambao hufanya shughuli zao pembezoni mwa barabara.
Alieleza haja ya kuandaa utaratibu wa kuwaweka wafanyabiashara katika mazingira mazuri pale wanapowaondoa kutoka eneo moja kwenda eneo jengine kwa ajili ya kufanya biashara zao.
Alipongeza hatua za kuanzisha mnada katika soko jipya la Jumbi hali ambayo imesaidia kwa kiasi kikubwa kuondoa msongamano wa wafanyabiashara masokoni.
Alisema ofisi ya Rais kupitia idara zake maalum za SMZ zimesaidia kwa kiasi kikubwa kulinda amani na utulivu nchini.
Alieleza kuwa utaratibu wa vikao vya kufanya tathmini na kuripoti (bango kitita), unatumika sehemu mbali mbali duniani na kwa upande wa serikali tokea alipouanzisha umepata mafanikio.
Alisema Zanzibar imepiga hatua kubwa ambapo mafanikio yaliopatikana ni pamoja na kukua uchumi na kufikia uchumi wa kati hatua ambayo imetokana na makusanyo mazuri ya mapato.
Aliipongeza ofisi hiyo na wafanyakazi wake huku akiwataka viongozi kuendelea kuchapa kazi na kuweka heshima ya nchi yao.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi, Seif Ali Iddi alimpogeza Dk. Shein kwa utaratibu wake huo pamoja na kuupongeza uongozi wa ofisi hiyo kwa juhudi walizozichukua huku akiwasisitiza kuimarisha miundombinu ya elimu, afya na kilimo.
Mapema Waziri wa wizara hiyo, Haji Omar Kheri, alisema ofisi imeendelea kuhudumia skuli 327 za maandalizi na msingi kwa kuhakikisha zinatoa huduma ya ufundishaji na kujenga mazingira mazuri ya kujifundishia.
Alisema ununuzi wa madaftari 4,624,846 kwa wanafunzi 325,009, madaftari 5,500 ya mahudhurio na kadi 50,000 za maendeleo ya wanafunzi umefanyika na kusambazwa kila wilaya za Unguja na Pemba.
Huduma za tiba na kinga ya afya ya msingi na huduma za afya ya mama na mtoto zimetolewa katika vituo 154 vya afya Unguja na Pemba chini ya usimamizi imara wa serikali za mitaa.
Alieleza kuwa uwajibikaji wa serikali za mitaa katika kusaidia miradi inayoibuliwa na wananchi umeongezeka ambapo kwa mwaka 2019/2020 miradi ya maendeleo 59 yenye thamani ya shilingi bilioni 1.7 imetekelezwa kwa upande wa Unguja na miradi 17 yenye thamani ya milioni 521.9 imetekelezwa Pemba.
Alieleza historia iliyoandikwa na Dk. Shein ya kuanzisha jiji la Zanzibar baada ya kufanya uteuzi wa Mkurugenzi wa jiji ambapo pia ofisi kwa kushirikiana na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Mji Magharibi iliratibu uchaguzi wa Meya na Naibu Meya na kuapishwa madiwani wa baraza la jiji.
Alipongeza hatua za Dk. Shein za kuridhia na kuzipandisha hadhi halmashauri za wilaya ya kaskazini ‘A’, kaskazini ‘B’ na halmashauri ya wilaya ya kati kuwa mabaraza ya miji.
Alisema usalama wa jiji la Zanzibar, mji wa Mkoani, Chake Chake na Wete umeendelea kuimarika kupitia utekelezaji wa mradi wa mji salama ambapo kwa mwaka 2019/2020 kazi ya uwekaji wa vizuizi vya kiusalama katika barabara kuu imefanyika kwa upande wa Unguja pamoja na kufuatilia matukio 256 yaliyoonekana katika kamera za kiusalama (CCTV).
Katibu Mkuu Kiongozi na Katibu wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Abdulhamid Yahya Mzee, alisema mikutano ya bango kitita, ina msaada mkubwa katika kujitathmini na kujipima na kueleza haja ya kuendelezwa.
Nao viongozi wa wizara hiyo walitoa pongezi kwa Dk. Shein kwa kuwafanya kuwa makini na kujitathmini katika utendaji wa kazi zao.