NA MWANAJUMA MMANGA
MAONYESHO ya siku ya wakulima yanatarajiwa kuzinduliwa leo huku rais wa Zanzibar Dk. Ali Mohamed Shein akitarajiwa kuwa mgeni rasmi.
Maonyesho hayo yanayofanyika chini ya usimamizi wa Wizara ya Kilimo, Maliasili, Mifugo na Uvuvi, yatafanyika kwa siku nne hadi Agosti 8 kwa upande wa Unguja wakati kwa upande wa Pemba kutafanyika maonyesho ya siku ya chakula duniani.
Naibu Waziri wa wizara hiyo, Dk. Makame Ali Ussi, aliyasema hayo alipokuwa akitoa taarifa kuhusiana na maonyesho hayo na kueleza kuwa wizara yake imeandaa mikakati ya kuwaimarisha wakulima ili wafaidike na mbinu za kilimo cha kisasa.
Maonyesho hayo yatafanyika katika viwanja vya Dole – Kizimbani kwa Unguja na Chamanangwe Pemba ambayo kikawaida hufanyika mwezi Oktoba, ikiwa ni shamrashamra ya siku ya chakula duniani, kwa mwaka huu yanafanyika kuanzia Agosti 6 hadi 10 ili kupisha harakati za uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba 28 mwaka huu.
Alisema miongoni mwa mikakati hiyo ni pamoja na kuwapatia mbinu za kisasa za kilimo wakulima, kuanzisha mashamba darasa, kuwapatia pembejeo kwa wakati na kutoa mafunzo ya namna ya kusarifu mazao ili kuongeza thamani na uzalishaji wa mazao.
Aidha alisema hatua hiyo itawasaidia wananchi wanaojihusisha na sekta ya kilimo kuinua kipato cha mtu mmoja mmoja na kuongeza upatikanaji wa chakula nchini.
Alifahamisha kuwa ni vyema wakulima waongeze kasi ya kulima kilimo cha mpunga ili kuokoa fedha zinazotumika kuagiza chakula kutoka nje ya nchi badala yake zisaidie katika sekta nyengine za kijamii.
“Maonyesho hayo yanalenga kuwaweka pamoja wataalamu wa kilimo na wakulima kuwapatia taaluma wananchi watakaofika huko ili kuona sekta ya kilimo inaimarika na kuongeza uzalishaji,” aliongeza Dk. Ussi.
Akizungumzia sekta ya uvuvi Dk. Ussi, alisema wana mpango wa kutoa taaluma zaidi kwa wakulima wa mwani kwa kuwapatia vihori kwa ajili ya kulimia mwani ili kuongeza uzalishaji wa zao hilo nchini.
“Tunafanya hivyo ili wakulima wetu wajifunze namna ya kutumia mbegu bora na nzuri lakini pia na kuzalisha mwani mwingi na kwa tija zaidi,” aliongeza Naibu Waziri huyo.
Hivyo aliwataka wakulima kutumia kilimo hai ambacho hakitumii mbolea na dawa zenye kemikali, badala yake kutumia maji sambamba na kufuata miongozo ya utabiri wa hali ya hewa ili kuongeza mchango wa sekta hiyo kutoka asilimia 20 ya sasa katika pato la taifa.
Zaidi ya wakulima 182, taasisi za serikali na taasisi binafsi zinatarajia kushiriki katika maonyesho hayo ambapo kiasi cha shilingi milioni 167 zinatarajiwa kutumika.
Kwa upande wake Msimamizi wa eneo la JKU (Meja) Ramadhan Ali Hasaan aliwataka wananchi na wakulima kushajiika kulima katika eneo dogo ambalo litaweza kulimwa na kupata mazao mengi.
Alisema pamoja na changamoto iliyojitokeza katika eneo hilo la kutokea mabadiliko ya hali ya hewa lakini wamejipanga kuhakikisha maonyesho ya mwaka huu yanaimarika zaidi.
Alisema kauli mbiu ya maonyesho ya mwaka huu ni “tudumishe amani na utulivu kwa maendeleo ya sekta ya kilimo”.