Asema zitatatua changamoto za wakulima

NA ABDI SHAMNA, IKULU

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Ali Mohamed Shein ameiagiza wizara ya Kilimo, Maliasili, Mifugo na Uvuvi kuhakikisha inajikita katika tafiti zinazohusiana na sekta za wizara hiyo.

Ametoa wito huo jana katika ufunguzi wa maonesho ya nane nane huko Chamanangwe, mkoa wa Kaskazini Pemba, ambapo alisema wizara hiyo lazima moja ya kipaumbele chake kiwe ufanyaji wa tafiti.

Alisema kupitia tafiti hizo, wizara itapata utaalamu mpya utakaowasaidia wakulima wa mazao mbalimbali, wavuvi na wafugaji kuondokana na changamoto zinazowakali.

Akitoa mfano, Dk. Shein alisema yanapotokea maradhi ya mifugo au mazao, wizara haipaswi kuishia kupiga dawa pekee, bali inatakiwa kutafuta chanzo cha maradhi hayo, kubuni njia za kuyaondoa na kuonesha njia ili yasiweze kutokea tena.

Alisema katika siku za hivi karibuni, wakulima wengi wamejikita katika kilimo cha mazao mbali mbali ya biashara ikiwemo matikitiki, tungule, matango na viazi, kupitia matumizi ya mbolea zenye kemikali.

Alisbainisha kwamba pamoja na uzuri wa kuendeleza kilimo hicho, ipo haja ya kufanya uchunguzi wa kitaalamu juu ya faida na hasara za kilimo cha aina hiyo, hasa katika afya ya udongo, ardhi, mazingira na virutubisho katika mazao yanayotokana na kilimo hicho.

Alifahamisha kuwa tangu asili kisiwa cha Pemba kinasifika kuwa na ardhi yenye rutuba, jambo lilolosababisha kupatikana mavuno mazuri kupitia matumizi ya mbolea za asili jambo ambalo hivi sasa limebadilika.

Alieleza kuwa watu wengi duniani wanaendelea kula vyakula vinavyotokana na kilimo hai kutokana na ladha ya asili ya vyakula hivyo pamoja na kuwepo uwezekano wa kupungua athari za kemikali.

Aidha, alisistiza umuhimu wa wizara hiyo kuwahamasisha wananchi juu ya uanzishaji wa mashamba ya viungo, ikiwa ni hatua ya kuvutia watalii na kuwapatia wananchi kipato cha kuendesha maisha yao.

Alisema mashamba hayo yanaweza kuwa sehemu za huduma za vyakula vinavyotumia viungo hivyo, ambapo wageni wataweza kuona uhalisia wa matumizi yake.

Katika hatua nyengine, kuanzishwa maonesho Dole kwa Unguja na Chamanangwe kwa Pemba, inatoa fursa kwa wananchi kutambua shughuli zinazofanywa na taasisi zinazoshiriki, ikiwa njia mojawapo ya kujitangaza na kupata masoko.

Alisema pamoja na wananchi kutambua umuhimu wa kufanyika maonesho hayo, idadi kubwa ya washiriki katika hafla hiyo ni uthibitisho wa kuunga mkono na kuthamini juhudi za serikali katika kuimarisha sekta za wizara ya Kilimo, Maliasili, Mifugo na Uvuvi.

Alisema serikali imejipangia mikakati kwa lengo la kuongeza uzalishaji kupitia mbinu bora, teknolojia ya kisasa, ujenzi wa miundombinu, utoaji wa thamani na upatikanaji wa masoko, mitaji na uhifadhi wa chakula, ili kuongeza tija, kukuza uchumi na kuondoa umasikini.

Dk. Shein alieleza kuwa hatua hiyo imeifanya serikali kuongeza bajeti ya kilimo, ambapo katika mwaka 2020/2021 imeongezwa kutoka shilingi bilioni 88.17 (2019) hadi shilingi bilioni 129.86 (2020), ikiwa sawa na asilimia 47.3.

Aidha, alisema hatua hiyo imeiwezesha serikali kutekeleza kwa mafanikio uwamuzi wa kutoa ruzuku ya asilimia 75 kwa ajili ya pembejeo za kilimo na huduma za matrekta kwa wakulima wa mpunga, jambo lilimeongeza mavuno ya mpunga kutoka tani 21,014 (2010) hadi tani 47,507 mwaka 2019.

Akigusia kilimo cha umwagiliaji maji, alisema juhudi zilifanyika kuendeleza kilimo hicho kwa kuendeleza mradi ya ujenzi wa miundombinu ya umwagiliaji katika mabonde ya Cheju, Kibokwa na Kilombero (unguja) na Mlemele na Makwarara kwa Pemba katika eneo la hekta 2,200.

Aidha alisema juhudi za kuiendeleza sekta ya Uvuvi zimefanyika, ikiwemo kuifufua kampuni ya Uvuvi ya Zanzibar (ZAFICO) kwa ununuzi wa boti mbili, ambapo tayari moja imefika nchini na nyengine inatarajiwa kuwasili mwezi ujao.

Kuhusiana na sekta ya mifugo, Dk. Shein alisema juhudi zimefanywa kuimarisha shughuli za ufugaji, ikiiwemo kuwapatia taaluma wafugaji, huduma za chanjo kwa mifugo ili kuwakinga wanyama dhidi ya maradhi.

Aidha, alisema wananachi wamehamasishwa kaunzisha vikundi vya ufugaji na kupatiwa bure ng’ombe 368 wa maziwa na mbuzi wa maziwa 720 ili kuendeleza ufugaji.

Dk. Shein alisema Serikali iko katika hatua za mwisho za makubaliano ya kuanzisha mradi wa ujenzi wa kiwanda kikubwa cha kusarifu mwani katika eneo la Chamanangwe kwa kushirikiana na kampuni ya “Ocean Fresh na Kapa Carageenan Nasuntara ya Indonesia”.

Alisema hatua hiyo itachochea kwa kiasi kikubwa ongezeko la bei ya mwani na hivyo kunufaika na kilimo hicho, akibainisha jitihada hizo zimewezesha bei ya zao hilo aina ya kotoni kuoongezeka hadi shilingi 1,800 kutoka shilingi 800 kwa kilo moja.

Katika hafla hiyo Dk. Shein alipata fursa ya kutembelea baadhi ya mabanda ya maonesho, yawemo ya Idara ya Uvuvi, Idara Klimo na wajaasiriamali na kupata maeleo juu ya shughuli mbali mbali zinaofanyika.

Mapema, waziri wa Wizara Kilimo, Maliasili, Mifugo na Uvuvi, Mmanga Mjengo Mjawiri aliwataka wananchi na vijana kujiajiri wenyewe na kutumia elimu inayotolewa katika maonesho hayo ili kuongeza uzalishaji.

Nae, Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo, Maliiasili na Mifugo, Maryam Abdalla Sadalla alisema kauli mbiu ya maonyesho hayo isemayo “Tudumishe amani navutulivu kwa maendeleo ya sekta ya Kilimo nchini’ inakwenda sambamba na mikakati na Ilani ya Uchaguzi wa CCM (2015-2020).

Alisema maonesho hayo yamewashirikisha washiriki 189 yakiwa ni suala la kitaifa ambapo watendaji kutoka Hlamashauri za Wilaya, pamoja Uongozi wa Wilaya na Mikoa walishiriki kikamilifu katika maandalizi yake.

Hayo ni maonesho ya tatu kufanyika kisiwani humo, ambapo yanafanyika yakienda sambamba na siku ya Chakula Duniani.