Apongeza wizara afya kwa utekelezaji majukumu

NA RAJAB MKASABA, IKULU

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Ali Mohamed Shein,  amesema dhamira ya serikali kujenga hospitali mpya huko Binguni wilaya ya Kati, upo kama ulivyopangwa.

Dk. Shein alieleza hayo jana ikulu mjini Zanzibar alipokutana na uongozi wa wizara ya Afya wakati ilipowasilisha utekelezaji wa mpango kazi wa mwaka 2019/2020 na mpango kazi wa mwaka 2020/2021.

Alisema mradi wa ujenzi wa hospitali hiyo ambao utaanza hivi karibuni,  utafanywa kwa kutumia fedha za ndani na kwamba utaanza mara tu wizara ya Fedha na Mipango itakapotoa fedha.

Alifafanua kuwa hospitali hiyo itakayokuwa na majengo 11, ni utekelezaji wa ilani ya Chama cha Mapinduzi, sera na mipango na kwamba yeye kwa upande wake ameshaamua ijengwe.

Aliipongeza wizara hiyo kwa uwasilishaji mpango kazi sambamba na utekelezaji wake na kuwapongeza viongozi na wafanyakazi wa wizara hiyo kwa kutekeleza vyema majukumu yao katika kuwahudumia wananchi.

Alisema kuwa viongozi wa wizara ya Afya wanafanyakazi zao kwa mashirikiano huku akitumia fursa hiyo kumpongeza waziri wa wizara hiyo  na viongozi wengine kwa kutoyumba katika kipindi cha maradhi ya corona.

Dk. Shein alisema mafanikio yaliyopatikana katika kukabiliana na ugonjwa wa  corona hapa nchini yametokana na kujiamini, kutoogopa na kuondoa hofu.

Aidha, alisisitiza kuwa wafanyakazi wa sekta ya afya wana kazi ya kutoa huduma kwa wananchi na kueleza serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imeamua huduma za afya kuwa bure.

Aliwataka wafanyakazi wa wizara ya Afya kuyasimamia maamuzi ya serikali kuhakikisha kuwa huduma za afya zinaendelea kutolewa bure na kusisitiza kuwa hakuna haja ya wananchi kuambiwa vyenginevyo.

Dk. Shein alisisitiza umuhimu wa kufanywa tafiti ili kuimarisha sekta hiyo, kwani suala hilo ni uwamuzi wa dunia nzima ambao umekuwa ukisaidia kwa kiasi kikubwa kuleta maendeleo.

Akizungumzia vikao vya kutathmini utekelezaji wa mpango kazi ambavyo vimekuwa vikifanyika katika kipindi chote cha uongozi wake, alisema kuwa vikao hivyo ambavyo ni vya mwisho katika muda wa uongozi wake, vimemsaidia kwa kiasi kikubwa kufuatilia utekelezaji wa mipango ya serikali katika wizara zake.