NA TATU MAKAME

HATIMAE mshitakiwa wa kesi ya ubakaji ya kumuingilia kinyume na maumbile na kumtorosha msichana wa miaka tisa aliye chini ya uangalizi wa wazazi wake, ameachiwa huru baada ya upande wa mashitaka kushindwa kuthibisha kosa katika mahakama ya mkoa Vuga.

Aliyeachiwa huru ni Mohamed Jecha Zidi (52) mkaazi wa Jang’ombe Wilaya ya Mjini Unguja.

Ilidaiwa kuwa mshitakiwa huyo alitenda makosa mawili kwa wakati mmoja, ambapo kosa la kwanza ni kumtorosha msichana kinyume na kifungu cha 150 (a) cha sheria namba 6 ya mwaka 2004 sheria ya Zanzibar.

Kosa la pili ni kumuingilia kinyume na maumbile, kinyume na kifungu cha 130 (a) cha sheria namba 6 ya mwaka 2004 sheria ya Zanzibar.

Akitoa maamuzi hayo, Hakimu Valentine Katema wa mahakama hiyo baada ya Mwendesha Mashitaka kutoka Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP), Ahmed Mohamed, kuwasilisha jadala la kesi hiyo mbele ya mashahidi waliofika kutoa ushahidi.

 Hakimu huyo alisema anatoa uamuzi huo, baada ya upande wa mashitaka kushindwa kuthibitisha kosa mahakamani hapo licha ya ushahidi uliotolewa na mashahidi mahakamani hapo.

Ilidaiwa kuwa mshitakiwa huyo, alitenda kosa la kumtorosha na kumuingilia kinyume na maumbile mtoto wa miaka tisa (jina linahifadhiwa), jambo ambalo ni kosa kisheria.

Mwendesha Mashitaka alisema, mshitakiwa huyo mnamo Oktoba 2016 alitenda kosa la kumtorosha mtoto huyo kumtoa Jang’ombe na kumpeleka nyumbani kwake kisha kumuingilia.

Kesi hiyo ilifunguliwa mahakamani hapo Machi 6 mwaka 2018.