NAIROBI, KENYA
TUME ya Maadili na kukabili ufisadi EACC, imesema ilipata idhini ya kufanya msako nyumbani kwa Gavana wa Kirinyaga Ann Waiguru kutoka Mahakama ya Hakimu ya Nyeri.
Kwa mujibu wa taarifa kutoka EACC, tume ilisema inatafuta stakabadhi zitakazosaidia kufanikisha uchunguzi wa madai kwamba Gavana Waiguru na baadhi ya maofisa wa Serikali ya Kaunti walilipwa shilingi milioni 23 kwa safari za nje ambazo hawakuzifanya.
Aidha,ilisema itaweka wazi matokeo ya uchunguzi wa msako unaoendelea kufanywa katika maboma na ofisi za Waiguru baada ya shughuli hiyo kukamilika.
Msako huo ulianza alfajiri huku pia wakichunguza Ofisi za Mkuu wa Wafanyakazi Sela Mugongo na Ofisa wa Fedha.
Waiguru anahusishwa na tuhuma mbalimbali ikiwemo utumizi mbaya wa ofisi, kupokea marupurupu ya shilingi milioni 10.6 za safari za nje ambazo anadaiwa kutozifanya, utoaji wa tenda wa shilingi milioni 50 kinyume na sheria na ununuzi wa gari la shilingi milioni 15 miongoni mwa nyenginezo.
Waiguru ambaye aliondolewa lawama na Seneti kufuatia ukosefu wa ushahidi wa kutosha dhidi yake, amekuwa akiwalaumu Wawakilishi waliopitisha hoja ya kumwondoa madarakani akisema kwamba wanatumiwa na mahasimu wake wa kisiasa.
Juhudi za Waiguru kutafuta mwafaka kati yake na viongozi hao ziliambulia patupu huku wakipunguza na kukataa kupitisha bajeti ya matumuzi ya ofisi yake na Naibu wake.
Hatua hii inasemekana kulemaza huduma za Serikali za kaunti ambapo wiki chache zilizopita Naibu wake Peter Ndambiri alikiri kwamba Kaunti ya Kirinyaga haina uwezo wa kukabili janga na virusi vya korona iwapo maambukizi yataongezeka.
Maofisa hao wa EACC, wanajaribu kutafuta stakabadhi zitakazo fanikisha uchunguzi wao dhidi ya madai mbalimbali yanayomwandama Gavana Waiguru.