BAMAKO,MALI

VIONGOZI wa Jumuiya ya kiuchumi ya Afrika Magharibi ECOWAS wamekutana jana kujadili mapinduzi ya kijeshi nchini Mali, yaliyomuondoa madarakani Rais Ibrahim Boubacar Keita.

Kwa muda mrefu jumuiya hiyo imekuwa ikijaribu kusuluhisha mgogoro huo kabla ya mapinduzi hayo.

Ofisa wa jeshi la Mali kanali Assimi Goita alitangaza kuwa ndiye kiongozi wa mapinduzi.

Umoja wa Afrika tayari uliisimamisha Mali kufuatia mapinduzi ya Jumanne,na kuungana na jumuiya nyengine za kimataifa ikiwemo Umoja wa Mataifa na ule wa Ulaya kulaani mapinduzi hayo.

Kundi la mataifa matano ya kanda ya Sahel limewataka wanajeshi walioongoza mapinduzi kumuachia Rais Keita na maofisa wengine wa Serikali yake wanaowashikilia.

Wanajeshi hao walisema kwamba wanapanga kuunda Serikali ya mpito ya kiraia itakayoandaa uchaguzi mpya.