BAMAKO,MALI
MAZUNGUMZO kati ya wawakilishi wa mataifa ya Afrika Magharibi na viongozi wa kijeshi wa Mali yameshindwa kufikia makubaliano ya jinsi ya kurejesha utawala wa kiraia nchini humo baada ya mapinduzi ya wiki iliyopita.
Mkuu wa Ujumbe wa Jumuiya ya kiuchumi ya nchi za Afrika Magharibi ECOWAS, Goodluck Jonathan alisema wamefanikiwa kufikia makubaliano katika baadhi ya masuala muhimu lakini walipeana muda wa kuyatafakari mengine ambayo hawakufikia mwafaka.
Mkwamo katika suala nyeti la kuirejesha Mali chini ya utawala wa kiraia uliibuka baada ya majenerali wa jeshi kutaka kupewa miaka mitatu ya kipindi cha mpito kuongoza nchi hiyo.
Mapinduzi ya Agosti 18 yalizitikisa nchi jirani na Mali, zinazohofia taifa hilo linalopambana na kitisho cha makundi ya itikadi na hali ngumu ya uchumi linaweza kutumbukia kwenye machafuko zaidi.