ANKARA,UTURUKI

BARAZA la Wataalamu barani Ulaya limemtaka Rais Tayyip Erdogan wa Uturuki kuchukuwa hatua dhidi ya mateso ya washukiwa mikononi mwa polisi.

Kamati ya baraza hilo inayojihusisha na kuzuwia utesaji ilisema kwamba imepokea malalamiko mengi juu ya mateso ya polisi kwa washukiwa, wakiwemo wanawake na watoto, wanaokuwa mikononi mwao.

Sehemu kubwa ya washukiwa hao ni wale waliofanya makosa madogo madogo kama ya madawa ya kulevya, ambao huteswa ili wakiri makosa.

Hata hivyo, Serikali ya Uturuki ilikanusha tuhuma hizo,Baraza hilo la Wataalamu wa Ulaya limeishutumu Uturuki kwa kuyaweka magereza katika hali mbaya, likiwemo gereza la Imrali, anakoshikiliwa kiongozi wa Wakurdi, Abdallah Ocalan.

Ripoti kama hizi kuhusu hali ya haki za binaadamu zinazotolewa na taasisi za Ulaya zina athari ya moja kwa moja kwenye jitihada za Uturuki kutaka uwanachama wa Umoja wa Ulaya.