KAMPALA,UGANDA

SHIRIKA  la chakula na kilimo la Umoja wa Mataifa (FAO), limesema idadi kubwa ya makundi ya nzige wa jangwani yanaweza kusafiri na kutishia mashamba,malisho ya wanyama na maisha ya watu eneo la Afrika Magharibi.

Makundi hayo ya nzige yaliyojikusanya katika eneo la pembe ya Afrika,hasa nchini Ethiopia na Kenya, tangu mwezi Januari mwaka huu yanaweza kuanza kusafiri katika wiki zijazo na kutishia usalama wa maeneo ya Afrika Magharibi.

FAO ilisisitiza kwenye ripoti yake kuhusu ufuatiliaji wa kitaifa wa nzige hao kuwa bado ni tishio, na hatua za kukabiliana nao ziko tayari kutokana na mfumo wa tahadhari ya mapema ya FAO.

Kwa mujibu wa taarifa ya ufuatiliaji wa nzige ya shirika hilo, makundi yaliyozaliana mwishoni mwa mwaka jana katika eneo la Afrika Mashariki sasa yanaelekea kwenye maeneo ya kuzaliana yenye joto, na nchi zilizoko magharibi mwa Pembe ya Afrika zinatakiwa kuwa makini.

Wiki iliyopita FAO pia ilionya kuwa nchi za Afrika Mashariki zinakabiliana na changamoto ya tishio la usalama wa chakula kutokana na changamoto tatu za mafuriko,COVID-19 na nzige wa jangwani.