NA LAYLAT KHALFAN

SERIKALI ya Mapinduzi Zanzibar, imesema itaendelea kuthamini juhudi zinazochukuliwa na watu wa Jamuhuri ya China katika kuimarisha sekta mbalimbali za maendeleo nchini .

Mkurugenzi wa Baraza la Manispaa Mjini, Said Juma Ahmada, aliyasema hayo katika hafla ya kupokea barakoa kutoka Manispaa ya Haicol nchini China, hafala ambayo ilifanyika katika baraza hilo, Malindi Mjini Zanzibar.

Alisema kupatikana kwa vifaa hivyo kutasaidia wananchi kufanya shughuli zao za kujiletea maendeleo ya kila siku, kwani wananchi wanatakiwa kuchukua tahadhari baada ya ugonjwa wa Corona kupungua hapa nchini, kwani baadhi ya nchi bado zinaendelea kusumbuliwa na ugonjwa huo thakili.

Aliwataka wananchi kufuata maelekezo yanayotolewa na wataalamu wa afya katika kujikinga na maambukizi mapya ya virusi vinavyosababishwa na maradhi ya Corona.

Naye Meya wa Manispaa wa Mji wa Zanzibar, Khatib Abrahman Khatib, alisema uhusiano uliokuwepo na watu wa China utaweza kuleta mafanikio mbalimbali katika nchi hususan katika sekta ya Elimu, Afya.

Akizungumza kwa niaba ya Meya wa Manispaa ya Hicol, Balozi Mdogo wa China Xie Xiaowu, alisema wataendelea kuisaidia Zanzibar katika nyanja tofauti,  ili iweze kupiga hatua zaidi kimaendeleo.

Jumla ya Barakoa 50,000 zimetolewa na Manispaa ya Haicol ya nchini China ambazo zitagaiwa kwa wafanyabiashara wa masokoni, vituo vya afya, pamoja na watendaji wa baraza la Manispaa Mjini.