LONDON,England
MLINDA mlango wa Manchester United, Dean Henderson, amesaini mkataba mpya na klabu hiyo hadi Juni 2025.

Mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 23 alitumia misimu miwili iliyopita kwa mkopo huko Sheffield United.

Siku ya Jumanne, Henderson alitajwa katika kikosi cha England kwa michezo ya Ligi ya Mataifa mwezi Septemba.

“Imani ya meneja na klabu wameonyesha kwangu kwa mkataba huu, inamaanisha mengi kwangu na nitaendelea na maendeleo yangu kama kipa.”

Alionekana mara 86 akiwa na ‘Blades’ baada ya kujiunga nao mnamo 2018, akiwasaidia kupanda Ligi Kuu ya England katika mwaka wake wa kwanza.

Msimu uliopita walimaliza nafasi ya tisa ya ligi hiyo ya juu huku Henderson akionesha kiwango kwa kuwa kipa chaguo la kwanza.

Henderson, ambaye ana chaguo la uongeza mkataba wake kwa mwaka mwengine, amekuwa na Manchester United tangu akiwa na umri wa miaka 14 na alipokea wito wake wa kwanza wa England mnamo Oktoba 2019.

“Tuko katika nafasi nzuri ndani ya idara ya walinda milango na hiyo inatupa ushindani wa maeneo ambayo tunatafuta kwenye kikosi”.
Wakati huo huo, meneja wa Liverpool, Mjerumani, Jurgen Klopp, amesema, kitendo cha Bayern Munich kuchukua taji la Ligi ya Mabingwa Ulaya ilikuwa ni bahati na ilibebwa zaidi na ratiba yake.

Klopp ambaye aliwahi kuwa mpinzani mkubwa wa miamba hiyo wakati anainoa Borussia Dortmund kuanzia mwaka 2008 hadi 2015, alianza kwa kuwapongeza kwa ubingwa huo, lakini, hakuacha kutoa mtazamo wake.

“Bayern walikuwa na bahati na hiyo ilitokana na aina ya ratiba yao ambayo ilikuwa inawafanya kuwa bora kwenye UEFA. Ukiacha hilo pia imekuwa ni kipindi ambacho wana timu bora na nzuri ambayo inajengwa na wachezaji vijana wenye uwezo mkubwa”, alisema.

Klopp alikuwa anazungumzia ratiba kama chanzo cha Bayern kufanya vizuri kwa vile Ligi Kuu ya Ujerumani ndio iliyokuwa ya kwanza kurejea mwezi Mei, baada ya kusimamishwa kwa hofu ya janga la ‘corona’.

Bayern ilimaliza ligi wakati timu pinzani ilizokuwa inacheza nazo bado zilikuwa na ratiba ya ligi huku Uefa yenyewe ikiwa na ratiba moja tu.

Inaelezwa jambo hilo liliifanya Bayern kuwa na muda mwingi wa kupumzika na kufanya mazoezi tofauti na wapinzani wake ikiwemo PSG ambayo ligi haikurejea.(Goal).