WASHINGTON,MAREKANI

WAZIRI wa zamani wa Mashauri ya Kigeni wa Marekani amesisitiza kuwa Serikali ijayo ya nchi hiyo inapasa kurejea katika mapatano ya JCPOA kwa sababu hatua hiyo ni kwa maslahi ya Washington.

Hillary Clinton alisema kuwa ni vyema Washington irejee katika mapatano ya JCPOA na ifanye juhudi za kulinda vizuizi vilivyowekwa katika miradi ya nyuklia ya Iran ili kuzuia mashindano ya silaha katika eneo. 

Joe Biden mgombea mkuu wa chama cha Democrat katika uchaguzi ujao wa Rais huko Marekani amekuwa akisisitiza kuwa Washington itarejea katika mapatano ya nyuklia ya Iran iwapo atashinda katika uchaguzi huo. 

Azimio lililopendekezwa na Marekani kwa ajili ya kuongeza muda wa marufuku ya vikwazo vya silaha dhidi ya Iran liligonga mwamba na kushindwa kupasishwa katika kikao cha Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa. 

Nchi 11 zilijizuia kupiga kura,Marekani na Jamhuri ya Dominican zilipiga kura ya ndio kuunga mkono azimio hilo na China na Russia zikalipinga.

Wanachama wa kudumu na wasio wa kudumu wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa ambao walijizuia  au kulipigia kura za hapana azimio hilo la Marekani dhidi ya Iran walisema kuwa walifanya hivyo wakiunga mkono mapatano ya JCPOA na kutokana na hatua zisizo za kisheria za Marekani.