HATIMAYE Ligi Kuu ya Zanzibar imefikia tamati kwa klabu ya Mlandege kufanikiwa kutwaa ubingwa baada ya kujikusanyia pointi 68, wakiivua KMKM iliyokuwa ikishikilia taji hilo.
Zanzibar Leo tunaungana na wapenzi wa soka wa Zanzibar kuipongeza timu hiyo ya Mlandege kwa

kufanikiwa kutwaa ubingwa huo waliokosa kwa zaidi ya miongo miwili.
Tunatoa pongezi hizo huku tukielewa kwamba ubingwa huo wa Mlandege haukuja kama dharura, bali uliandaliwa kwa uwekezaji na mipango mizuri ya uongozi.

Bila ya shaka, wadau wa soka wataendelea kuamini dhana ya kwamba ili soka lichezwe vizuri kamailivyofanya Mlandege, uwekezaji wa kutosha nao haukwepeki katika kufikia malengo.
Tunajua kwamba jitihada zilizofanywa na viongozi, mashabiki na mfadhili wa klabu hiyo, ndiyo hasa zilizochochea ubingwa wa timu hiyo.

Tunasema hivyo tukimaanisha kwamba Mlandege ilifanya usajili mzuri na mkubwa ulioiletea wachezaji wenye uwezo wa kupambana viwanjani na kupata matokeo chanya.
Kwetu sisi Zanzibar Leo licha ya pongezi hizi, lakini, tunaendelea kutoa rai kwa wafanyabiashara mbalimbali
kujitokeza na kudhamini timu hizi za ligi kuu ili kuongeza ushindani kwenye michuano hiyo mikubwa ambayo ndiyo hutoa mwakilishi wa kimataifa.

Klabu zetu zimekuwa zikipaza kilio chao cha kukosekana kwa udhamini kwenye ligi hiyo kubwa nchini ambacho kinatokana na namna zilinavyojikuta zikicheza ligi hiyo kwenye mazingira magumu hasa zinapokuwa nje ya vituo vyao Unguja na Pemba.
Lakini, pamoja na vilio hivyo, bado klabu ziliweza kucheza ligi hiyo kwa ushindani mkubwa hadi kupatikana kwa bingwa ambaye atatuwakilisha kwenye michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika mwaka ujao.

Ni ukweli usiopingika kuwa Shirikisho la Soka la Zanzibar (ZFF), linapita kwenye kipindi kigumu cha kusimamia ligi hiyo kutokana na kutokuwepo kwa mdhamini rasmi na hivyo kuzifanya klabu kubeba mzigo mzito wa ushiriki wao.
Sote ni mashahidi kuwa klabu zetu hazipo vizuri kiuchumi na zinaendeshwa kupitia michango ya mashabiki au viongozi wanaoziongoza hali ambayo kidogo ingeliweza kuweka rehani ushiriki wao pale michango itakapokosekana.

Hivyo, tunaamini kupatikana kwa mdhamini ambaye kwa kiasi fulani atasaidia uendeshaji wa ligi hiyo na klabu kuweza kushiriki bila ya gharama kubwa, ni miongoni mwa mambo yanahitaji kufanyiwa kazi kwa kadri ya iwezekanavyo.

Ni jambo zuri kuliona soka likichezwa kwenye utaratibu unaokubalika viwanjani huku wachezaji wakitimiza majukumu yao jambo ambalo litaifanya ligi kuwa ya ushindani zaidi badala ya kuonekana ligi iliyokosa dira.

Kama ambavyo wanafalsafa wa kiswahili wanavyosema kuwa mchezo ni gharama, basi sote tulione hilo kwa kuiunga mkono ZFF iweze kufanikiwa kupata mdhamini kwa ajili ya maendeleo ya soka yetu.

Sasa tufikie mahali na kuliona hili ni letu sote kwa njia moja au nyengine ili siku ya mwisho ligi yetu iwe na udhamini utakaongeza chachu ya mafanikio kwa ajili ya vijana wetu wa baadaye.
Hongera Mlandege, Zanzibar yenye mafanikio ya soka inawezekana.