NA ARAFA MOHAMED
WANANCHI wametakiwa kukubaliana na utaratibu ulioweka katika Hospitalii kuu ya Mnazi Mmoja, wakati wanapoingia kuangalia wagonjwa wao.
Msemaji Mkuu wa Hospitali hiyo, Hassan Makame Mcha, alieleza hayo kufuatia malalamiko ya wanachi ya kuzuiliwa kuingia Hospitali hapo, alipokuwa akizungumza na mwandishi wa habari hizi Ofisini kwake Mnazi Mmoja Mjini Zanzibar.
Alisema, lengo la kuweka utaratibu huo na kuruhusu watu kuingia wawili wawili Hospitalini hapo ni kuondoa wingi wa watu kutoka na Hospitali hiyo kuwa ni ya Rufaa, haitakiwi kuwa na zogo la watu wengi kwa hali za wagonjwa.
Alifahamisha kuwa utaratibu huo ulipangwa kabla ya kipindi cha maradhi ya Corona, lakini ulianza kutumika wakati wa maradhi hayo kutokana na mkusanyiko wa watu kuwa wengi hospitali hapo.
Aidha, alisema kuwa mabadiliko yoyote yanakuwa magumu kwa siku za mwanzo hivyo amewaomba wananchi hao, kufuata maelekezo yanayotolewa ili waweze kupatiwa huduma zilizo bora.
“Mabadiliko yanatabu kwa siku za mwanzo lakini wananchi wanapaswa wakubaliane na hali hiyo, kwa sababu hospitali ya mnazi mmoja ni tofauti na hospitali nyengine, haitakiwi kuwa na msongamano” alisema.