NA MWANDISHI WETU
“USANII umenisaidia kunifikisha mbali ikiwemo kujiamini na kuweza kuzungumza sehemu yoyote mbele za watu, hiyo kwangu ni faraja kubwa”.

Hayo ni maneno ya msanii maarufu wa muziki wa taarab asilia visiwani hapa anayetamba na kundi la Culture na kikundi cha taifa, Iddi Suwedi maarufu ‘Mpendwa na wengi’.

Msanii huyo aliyejizolea sifa nyingi kupitia utunzi wake wa mashairi, utiaji wa muziki na hata uimbaji wake ambao wengi huwafanya wayumbe yumbe kwenye viti vyao na wengine kushindwa kuvumilia na kuanza kuserebuka.

Gazeti la Zaspoti ilibahatika kukutana na msanii huyo na kutaka kujua alipoanzia na mpaka alipofikia katika sanaa ya muziki wa taarab asilia visiwani Zanzibar.

Msanii huyo, alieleza, alianza rasmi sanaa tokea akiwa kijana mdogo huko kijijini kwao Kizimkazi Mkunguni wilaya ya Kusini Unguja ambapo wakati huo skuli yao ilianzisha kikundi ambacho kilikuwa kikiimba nyimbo za taarab kwa kutumia ngoma.

Alisema kikundi hicho kilikuwa kinajulikana kwa jina la ‘Young Pioneers’ ambacho kilianzishwa baada ya Mapinduzi matukufu ya Zanzibar mwaka 1964 na kilikuwa kikifanya maigizo pamoja na kuimba.

Msanii huyo alisema, mbali na kuanzia huko, lakini, amerithi kutoka kwa mama ake mzazi ambae alikuwa akiimba katika kikundi cha ‘Mikunguni Social Club’. “Fani ya muziki niliianza zamani tangu nikiwa mdogo huko nyumbani kwetu Kizimkazi,lakini, pia nimerithi kwa mama yangu mzazi”, alisema.

Msanii huyo alisema wakati skuli zikiwa zinafungwa alikua anakuja mjini kutembea kwa mama yake na alikua akimchukua kwenye mazoezi ya kikundi chao na yeye hupata nafasi ya kujifunza zaidi.

Alisema baada ya kumaliza elimu ya msingi na kulazimika kuhamia mjini kwa ajili ya masomo katika skuli ya Lumumba mwaka 1968, alijiunga na kikundi cha maigizo na kuimba cha ‘Dramatic Society’cha skuli ambacho kilikuwa kinaongozwa na mwalimu wa uchoraji,marehemu Iddi Abdallah Farhan.

Alisema mwaka 1969 alijiunga rasmi na kikundi cha Mikunguni wakati huo alikua kidato cha pili na kukutana na wasanii wengi mahiri akiwemo marehemu Issa Kiwete, Fatma Usowanoti,Haji Mbilikasorobo, Khadija Rajab, marehem Issa Matona,mama yake mzazi na wengine wengi.

Akiwa katika kikundi hicho cha Mikunguni aliimba nyimbo moja iliyojulikana kwa jina la ‘Baiskeli ya kukodi’ iliyotungwa na Ali Ramadhan.

Baadhi ya beti zilizomo katika nyimbo hiyo ni pamoja na
‘Baiskeli ya kukodi, Naapa sipandi tena
Neno hili naahidi, Na nyinyi mtaniona
Kama tavunja ahadi,Anihukumu rabana

Jambo lilonichukia, Kwanza heshima haina
Wewe utaipandia ,Wende nayo kwa kutuna
Kumbe utompitia, Na yeye kapanda jana”.

Msanii huyo alieleza baada ya nyimbo hiyo pia aliimba nyimbo nyengine iliyokuwa inaitwa ‘Chozi la damu’ ambayo aliitunga na kuimba yeye mwenyewe.

Alisema baadae kuundwa kikundi cha taarab cha taarab cha Wilaya ambacho kilikusanya vikundi kadhaa vya Ng’ambo kikiwemo kikundi cha Mikunguni,Kidongochekundu, Mkadara,Gulioni,Shaurimoyo ili kupatikana ili kupatikana wasanii watakaojiunga na kundi la mila na utamaduni.

Gwiji huyo alisema kutokana na kipaji chake kuwavutia majaji waliokuwa wakiwashindanisha, alifanikiwa kujiunga na kundi hilo,lakini kutokana na wakati huo alikuwa mwanafunzi alilazimika kuachana na mambo hayo na kuendelea na masomo.

“Nilifanikiwa kujiunga na kundi la mila na utamaduni, lakini, mwalimu wangu marehemu Iddi Farhan, alinishauri niachane na mambo hayo na niendelee na masomo,”alifahamisha.
Alisema akiwa mwanafunzi aliendelea na kuimba na kikundi cha Mikunguni na huko Mila na Utamaduni alikuwa anakwenda kwa ajili ya kuwapa mazoezi wenzake.

Msanii huyo alisema mara baada ya kumaliza masomo alijiunga rasmi na kundi la Culture Musical Club lenye maskani yake Vuga mjini Unguja, mwanzoni mwa mwaka 1974 ambapo kundi hilo hakudumu nalo kutokana na kuondoka nchini kwenda Nairobi kwa ajili ya masomo.

“Nilishindwa kuendelea na sanaa kutokana na kulazimika kwenda Nairobi kusoma kwa muda wa miaka mitatu na baadae nilipomaliza masomo nilienda kufanya kazi Arusha na baadae nikahamia Pemba kwa muda wa miaka 10”, alisema.

Iddi akiwa kisiwani Pemba alikwenda kujiunga na kikundi cha taarab cha Chake Chake ambapo kikundi hicho kilimfanya achaguliwe kujiunga na kikundi cha taifa.

Alieleza akiwa kisiwani Pemba aliimba nyimbo maarufu ya marehem Issa Matona inayojulikana kwa jina la ‘Siri’ ambapo baaade nyimbo hiyo ilifungiwa.
Alisema mara baada ya kurudi Unguja mwaka 1983 alirejea tena rasmi ndani ya kundi lake la Culture alikutana na wasanii wengi mahiri na yeye alibakia kuwa muitikiaji na kuwa mpiga ala.

“Nilipojiunga tena na Culture nilikutana na wasanii wengi mahiri akina marehem Sami Haji Dau,Mwapombe Khiyari, marehemu Mwalim Abdallah na wengine wengi,hivyo mimi nilikosa nafasi ya kuimba hivyo nikabakia kuwa muitikiaji na mpiga ala”, alisema.

Msanii huyo, alisema, baadae alipata kazi jijini Dar es Salaam akiwa mwalimu wa masuala ya ‘digital’ambapo mwaka 1992 alirudi nyumbani akiwa na nyimbo maarufu inayotamba visiwani humu inayojuliakana la ‘Kweli Nnae’.


Alisema alipofika kwanza ilikuwa vigumu kukubaliwa kuimba nyimbo hiyo iliyotungwa na marehemu Mzee Haji na kuwekwa muziki na marehemu, Abass Machano.

“Nilionekana bado ni msanii mchanga sina uwezo wwa kuimba ikabidi nyimbo ile apewe Sada Mohammed, kutokana na yeye alikua tayari kishaanza kuimba,lakini, niliombewa na nikaimba mimi mwenyewe”,alisema.

Baadhi ya maneno katika nyimbo hiyo ni kama hivi :-

Kakweleza milima ilo na miti akapanda,Vikwazo havimpingi
Kachunguza kagundua kwa dhati nnampenda, Huba nnazo kwa wingi
Akajaza kuniteua kwa ridhaa roho tanda,Kapendezewa siringi

Kiitiko
Nawambia mashangingi, Ndio sasa amekua wangu
Nyinyi muwe maji ya mtungi,Mimi nimeshusha kiu yangu”.

Baada ya kuimba nyimbo hiyo na kumpatia umaarufu mkubwa ndipo akaendelea nyimbo nyengine ikiwemo
‘Kinachowasumbueni, Unalo, Bado nnae, Siri na nyengine nyingi ambazo zinafika nyimbo 22.

Msanii huyo ambae bado anaimbia katika kundi la Culture pamoja na kikundi cha Taifa anasema hajaona matatizo yoyote yaliyomkabili tangu ajiunge na fani hiyo .
Juu ya faida, Suwedi, alisema zipo nyingi ikiwemo kutembea nchi mbali mbali duniani na pia kuheshimika miongoni mwa wanajamii.

Alisema katika kuimba kwake anavutiwa na waimbaji mbali mbali waliokuwa hai na wengine waliotangulia mbele ya haki ambapo aliwataja ni pamoja na Rukia Ramadhan, marehemu Khadija Baramia na msanii wa zamani ambae wengi hawamfahamu kwa sasa ni Bi Mwanajuma Ali.

Msanii huyo alisema ipo tofauti kubwa kati ya taarab asilia na taarab ya kisasa ambapo alisema ya kisasa inatumia ala za moto.

“Ingawa tupo kwenye biashara, lakini, taarab ni ile ya asili pekee maana hii ya sasa haitumii ala za kizamani pia hauendani na maadili yetu, wanatunga nyimbo za matusi na hazipendezi katika jamii yetu,”alisema.

Akizungumzia juu ya muziki kunasibishwa na dhana ya uhuni, msanii huyo alipinga na kujitolea mfano yeye mwenyewe na kusema kwamba kama muziki angekuwa yeye muhuni lakini mpaka leo hajakuwa muhuni.

“Muziki sio uhuni,uhuni mtu kutaka mwenyewe,nawashangaa hao wanaosema kuwa muziki uhuni wakati kuna wahuni na wala si wasanii wa nyimbo wala fani nyengine yoyote,”alisema.

Gwiji huyo wa muziki wa taarab alisema katika fani ya sanaa na akiwa ndani ya kundi la Culture amefanikiwa kushika nyadhifa mbali mbali ikiwemo Katibu Mwenezi, Msaidizi Mkurugenzi, Mkurugenzi Mkuu na Naibu Mwenyekiti.

Suwedi,alisema, katika mambo ya sanaa,watoto wake wawili wamefuata nyayo zake ingawa mmoja amejikita zaidi katika uigizaji na nyimbo za bendi na mmoja ndie amefuata nyayo zake kuimba taarab.

“Mwanangu Ramadhan almaaruf ‘Mzee Nnawie’ yeye amejikita zaidi katika uigizaji, muziki sio sana, lakini Mustafa yeye amefuata nyayo zangu hasa,”alifafanua.

Aidha alitoa ushauri kwa wasanii wenzake kuangalia wanakotoka ili wasije kuharibikiwa hapo baadae kwa kutumia tungo ambazo hazifuati maadili ya Kizanzibari

Pia aliishauri Ofisi ya Hakimiliki Zanzibar (COSOZA), kubadilika na kuchukua hatua kwa wasanii wanaoiba kazi za watu bila ya ridhaa za wenyewe.

Iddi Suleiman Suwedi,alizaliwa mwaka 1952 huko kijijini kwao Kizimkazi Mkunguni akiwa mtoto wa mwisho katika familia ya watoto watatu mmoja wa kike na wawili wakiume.

Elimu yale aliianzia mwaka 1956 hadi mwaka 1967 katika Skuli ya Kizimkazi na baadae kujiunga naskuli ya Sekondari ya Lumumba hadi alipomaliza kidato cha sita na kuendelea na masomo katika vyuo mbali mbali.

Msanii huyo mbali na kuwa msanii pia aliwahi kuwa mfanyakazi wa Kampuni ya Simu Tanzania (TTCL) kwa muda wa miaka 31 na kufikia kuwa Mkurugenzi wa Kanda wa TTCL na baadae pia aliwahi kushika wadhifa wa Mkurugenzi na Mpigachapa Mkuu wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar.