NA MADINA ISSA

MKUU wa Jeshi la Polisi Tanzania, Simon Sirro, amewataka viongozi wa dini kuendelea kufanya kazi ya kuhubiri amani na utulivu katika nyumba zao za ibada, ili amani iliyokuwepo iendelee kudumu.

Akizungumza katika kikao cha pamoja na wajumbe wa kamati ya amani Zanzibar wakiwemo viongozi wa dini kikao ambacho kimefanyika katika ukumbi wa Mfuko wa hifadhi ya jamii ZSSF ulipo Kariakoo mjini Unguja.

Alisema, ili amani iendelee kudumu katika nchi, viongozi wa dini hawana budi kuendelea kuhubiri na kuwapatia elimu waumini wao, ili amani iendelee kutawala nchini.

Aidha alisema, katika kuelekea kipindi cha uchaguzi kumekuwepo na baadhi wanaofumba macho yao kuona amani iliyokuwepo kwa kutaka kuichafua amani iliyokuwepo, jambo ambalo halikubaliki katika nchi na mataifa mbalimbali.

Hivyo, aliwasisitiza wananchi kutojiingiza katika machafuko kipindi cha kuelekea uchaguzi na wakati wa uchaguzi, kwani jeshi la polisi litamshughulikia kila atakayebainika kufanya vurugu kwa kuchukuliwa hatua stahiki kwa mujibu wa sheria.

“Viongozi wa dini muendelee kulisaidia taifa hasa katika mahubiri yenu hasa kipindi hichi, na sisi jeshi tupo imara katika kuhakikisha amani inaendelea kutawala nchini” alisema.