BEIRUT,LEBANON

MKURUGENZI  Mwandamizi wa Mfuko wa Fedha wa Kimataifa IMF Kristalina Georgieva,ameitaka jamii ya kimataifa na nchi rafiki za Lebanon ziisaidie nchi hiyo kupunguza hasara iliyotokana na mripuko mkubwa uliotokea siku ya Jumanne katika bandari ya Beirut.

Mkurugenzi alisema hilo la kimataifa linatafuta njia zinazowezekana kwa ajili ya kuwasaidia watu wa Lebanon kukabiliana na mkasa huo.

Pamoja na hayo katika hatua ya uingiliaji wa mambo ya ndani ya Lebanon, Georgieva alisema kuwa Serikali ya Beirut inapasa kubuni mpango madhubuti wa kutatua mgogoro uliopo wa kiuchumi na kuimarisha misingi ya kuwajibika na kuvutia imani ya wananchi wa nchi hiyo.

Mwezi uliopita pia Serikali ya Lebanon ilianzisha mazungumzo na IMF kwa ajili ya kupata mkopo wa kukabiliana na kuenea kwa virusi vya corona na kutatua matatizo ya kiuchumi ya nchi hiyo, jambo ambalo lilishurutishwa kwa Serikali ya Beirut kutekeleza marekebisho ya kiuchumi yatakayoziridhisha nchi za Magharibi.

Matamshi ya karibuni ya Georgieva yalitolewa katika hali ambayo Marwan Aboud, Ganava wa Beirut alikisia hasara iliyosababishwa na mripuko wa karibuni kuwa kati ya dola bilioni kumi hadi 15.

Mripuko mkubwa ulitokea katika bandari ya Beirut ambapo kwa mujibu wa takwimu za karibuni,watu zaidi ya 157 walipoteza maisha na wengine karibu 5000 walijeruhiwa.