NA AMEIR KHALID

BALOZI Mdogo wa India anayefanya kazi zake Zanzibar, Bhagwant Singh, amesema serikali ya India inaendelea kuchukua juhudi za kukabiliana na janga la ugonjwa wa corona, ambapo umesababisha athari kubwa nchini humo.

Balozi Bhagwant alitoa kauli hiyo jana alipokuwa akizungumza na wananchi wa Zanzibar wenye asili ya India, kwenye hafla ya kuadhimisha miaka 74 ya uhuru wa nchi hiyo, iliyofanyika ofisi za ubalozi huo uliopo Migombani.

Alisema watu wengi wanaunga mkono juhudi za serikali ya India katika kukabiliana na ugonjwa huo na wamekuwa wakipongeza mafanikio waliyoyatapata hasa ikizingatiwa ukubwa wa tatizo hilo nchini humo.

Alisema taifa la India lina deni kwa madaktari, wauguzi na wafanyakazi wengine wa sekta ya afya ambao wamekuwa mstari wa mbele kwenye mapambano ya kutokomeza ugonjwa huo wa kuambukiza.

“Kwa bahati mbaya, wengi wao wamepoteza maisha, wao ni mashujaa wetu wa kitaifa, kutokana na kuwapambania wananchi wao kutokana na corona wanastahili sifa sana’’, alisema.

Alisema serikali inaendelea kutoa misaada kwa wananchi wake ikiwemo kuwapatia chakula, hali ambayo itahakikisha hakuna familia inayokosa ambapo mpango wa usambazaji wa chakula utafanyika hadi mwishoni mwa Novemba 2020.

Alisema lengo ni kutoa msaada kwa watu 80 wa kila mwezi. Ili kuhakikisha kwamba, majimbo yote yanakuwa chini ya mpango huo.

Aidha alifafanua kuwa mbali na juhudi za ndani ya nchi, lakini pia serikali imeelekeza nguvu zake kusaidia nchi nyingine katika mapambano dhidi ya Covid- 19.

‘’Tumekuwa mstari wa mbele katika kutoa misaada ya kikanda na ya kimataifa juu ya janga hili’’, alisema.

Alisema anaamini kuwa katika mapambano dhidi ya Covid- 19, maisha na njia ya kuishi kwa wote ni muhimu, hivyo wanaangalia shida iliyopo kama fursa ya kuanzisha mageuzi ya kuinua uchumi kwa faida ya wote, hasa wakulima na wafanyabiashara wadogo.

Katika hatua nyingine balozi huyo alisema wakati India inapata uhuru, wengi walitabiri kwamba nchi hiyo ingeshindwa kupata demokrasia ya kudumu, lakini wamefanikiwa kwa kiasi kikubwa na imekuwa nchi yenye demokrasia ya kuigwa duniani.