NEW DELHI, INDIA

BARAZA  la Maulamaa wa Kiislamu wa India limeitaka Serikali iwachukulie hatua kali na ya haraka waliomvunjia heshima Bwana Mtume Muhammad SAW.

Mkuu wa Baraza la Maulamaa wa Kiislamu wa India Sayyid Muhammad Othman alitaka watu waliomvunjia heshima Bwana Mtume SAW wapewe  adhabu na akaongeza kuwa, hiyo ndio njia pekee itakayoweza kupoza hisia zilizotiwa machungu za Waislamu na kudhamini amani ya nchi.

Maulana Sayyid Othman alibainisha kuwa, Bwana Mtume Muhammad SAW anaheshimiwa na jamii yote ya Waislamu na kumvunjia heshima yeye ni sawa na kuwatusi na kuwavunjia heshima Waislamu milioni 200 wa India.

Kiongozi huyo wa Baraza la Maulamaa wa Kiislamu wa India alieleza kwamba,Serikali ya Waziri Mkuu Narendra Modi inapaswa kuzuia vitendo vya kuyavunjia heshima matukufu ya Kiislamu vyenginevyo, vitendo vya aina hiyo vitasababisha mpasuko mkubwa zaidi wa tofauti ndani ya nchi hiyo.

Hivi karibuni,mbunge mmoja wa chama tawala cha BJP alituma maelezo katika mtandao wa kijamii wa Facebook wa kumvunjia heshima Bwana Mtume Muhammad SAW.

Waislamu wa India walioghadhibishwa na kitendo hicho kichafu walifanya maandamano ya kukipinga, lakini ukandamizaji uliofanywa na polisi ulipelekea Waislamu watatu kuuawa.