TEHRAN,IRAN

IRAN imewakamata raia wake watano kwa tuhuma za kuzifanyia upelelezi Israel, Uingereza na Ujerumani.

Idara ya Mahakama ilisema kuwa raia wawili kati ya raia hao watano wamehukumiwa na kupewa kifungo cha Gerezani.

Msemaji wa Idara ya Mahakama Gholam Hossein Esmaili alisema katika mkutano na waandishi habari kuwa katika miezi ya hivi karibuni, Wairan watano ambao walikuwa wakizifanyia upelelezi nchi za kigeni walikamatwa.

Esmaili alisema miongoni mwa waliokamatwa ni Shahram Shirkhani aliyekuwa akiifanyia upelelezi Uingereza na alijaribu pia kuajiri baadhi ya maofisa wengine wa Iran ili wakifanyie kazi kikosi cha upelelezi cha Uingereza cha M16.

Shirkhani alitoa maelezo ya siri kuhusu benki kuu ya Iran pamoja na kandarasi za Wizara ya ulinzi ya nchi hiyo.

Aidha, alitiwa hatiani na kupewa hukumu ya kifungo gerezani.