LONDON, England
KLABU ya ligi daraja la kwanza England ya Watford imethibitisha kumteua, Vladimir Ivic kama kocha wao mkuu mpya.
Kocha huyo mwenye umri wa miaka 43, amekubali mkataba wa mwaka mmoja huku kukiwa na chaguo la kuongeza mwaka mwengine na klabu hiyo.

Meneja huyo wa zamani wa klabu ya Maccabi Tel Aviv amerithi mikoba iliyoachwa na Nigel Pearson ambaye alitimuliwa akiwa na michezo miwili kabla ya msimu kumalizika.
Watford iliteremka kutoka Ligi Kuu ya England baada ya kupoteza mchezo dhidi ya Arsenal na mchezaji wa zamani, Hayden Mullins, akiwa kocha wa mpito.

Matokeo hayo yalihitimisha miaka mitano kwenye ligi hiyo ya juu kwa ‘Hornets’, ambao walicheza fainali ya Kombe la FA mwaka 2019.

Ivic ni bosi wa nne wa muda kamili wa Watford katika miezi isiyopungua 12 huku Javi Gracia na Quique Sanchez Flores wote walitimuliwa katika wiki za kwanza za msimu uliopita, na kusababisha Pearson kuwasili Disemba.

Alikuwa wakala wa bure baada ya kuiongoza Maccabi Tel-Aviv kutwaa mataji mawili mfululizo ya ligi huko Israeli na pia hapo awali aliinoa klabu ya Uigiriki ya PAOK ambayo ilishinda kombe la nyumbani.
(BBC Sports).