NA MWANDISHI WETU

TUME ya uchaguzi Zanzibar (ZEC) imeeleza kuwa itaendelea kusimamia sheria na kanuni za uchaguzi katika utekelezaji wa majukumu yake kinyume na inavyodaiwa na baadhi ya viongozi wa vyama vya siasa.

Mwenyekiti wa tume hiyo Jaji Mkuu Mstaafu Hamid Mahmoud Hamid alieleza hayo wakati wa kusaini kanuni za maadili ya uchaguzi katika ukumbi wa Sheikh Idriss Abdulwakil Kikwajuni, Zanzibar.

Alisema kabla ya kufanyika kwa uchaguzi, tume inatakiwa kuwa daftari la wapiga kura lililo safi hivyo hatua ya kuondolewa kwa wapiga kura walioshindwa kujihakiki ipo kisheria kwa kuwa walikosa sifa za kubaki katika daftari hilo.

Alieleza kuwa madai kwamba watu hao waliondolewa kwa kuwa ni wafuasi wa chama kimoja cha siasa sio sahihi bali ni kutokana na kushindwa kuhakiki taarifa zao na kutopinga kuondolewa kwao.

“Kwa mujibu wa kifungu cha 32 cha sheria ya uchaguzi namba 4 ya 2018 orodha ya wapiga kura waliopoteza sifa iliwekwa wazi kwa muda wa siku 7 na baada ya hapo waliondolewa kwa wale ambao hawakujitokeza kupinga kuondolewa kwao,” alieleza jaji Mahmoud.

Aidha Mwenyekiti huyo aliwakumbusha viongozi wa vyama hivyo kufungamana na kanuni za maadili walizotia saini ili kuwa na uchaguzi bora na kuimarika kwa Amani na utulivu wakati wote.

Awali akifafanua swala la kuondolewa kwa wapiga kura hao, Mkurugenzi wa uchaguzi ZEC Thabit Idarous Faina alieleza kuwa hatua hiyo ni ya kawaida na kwamba inafanyika kwa kuzingatia matakwa ya sheria.

“Katika kila uchaguzi hatua hii hufanyika kwani kutoka uchaguzi mmoja na mwengine kuna mambo mengi hutokea yanayopelekea watu walioandikishwa kupoteza sifa za kubakia katika daftari,” alieleza Faina.

Alifafanua kuwa katika uchaguzi wa 2010 wapiga kura 92,000 waliondolewa, mwaka 2015 walioondolewa walikuwa zaidi ya 100,000 ambapo kwa mwaka huu walioondolewa ni 82,263 wanawake 44,017 na wanaume 38,246.

Akizungumza baada ya vyama 18 kati ya 19 vya siasa vyenye usajili wa kudumu kusaini kanuni hizo, Naibu Msajili wa vyama vya siasa Mohammed Ali Mohammed alieleza kuridhishwa na ushirikishwaji wa wadau katika maandalizi ya uchaguzi jambo linaloashiria kuwa na uchaguzi bora.

Aliwataka viongozi wa vyama vya siasa na wadau wengine wa uchaguzi kuzingatia kanuni hizo na kufuatisha vitendo ili lengo la kuwa na uchaguzi wa amani lifikiwe.

“Utiaji saini huu ni vyema uendane na matendo kinyume chake ni kuzisaliti dhamira zenu na muda mliotumia kuziandaa jambo ambalo sio lengo la tume wala serikali,” alieleza Mohammed.

Mbali ya viongozi wa vyama vya siasa tume, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya nchi Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais Abdallah Hassan Mitawi alitia saini kwa niaba ya serikali huku Mwenyekiti wa kamati ya maadili wa ZEC Jaji wa mahakama kuu ya Zanzibar Khamis Ramadhan Shaaban aliweka saini kwa niaba ya tume.

Wakizungumza baada ya utiaji saini huo viongozi wa vyama vya siasa waliwahakikishia wananchi kuwa watazingatia kanuni, sheria na katiba katika hatua zote za uchaguzi na kuwaomba wadau wengine kuweka uzalendo.

Walisema kuna haja ya wadau hao kutambua kuwa uchaguzi ni njia ya kuimarisha uzalendo hivyo usitumike kuwagawa watu.

Utiaji saini huo ni sehemu ya maandalizi ya uchaguzi mkuu wa Zanzibar utakaofanyika Oktoba 28 ambao utahusisha uchaguzi wa Rais wa Zanzibar, Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi na Madiwani kwa uchaguzi unaosimamiawa na ZEC sanjari na uchaguzi unaosimamiwa na Tume ya Taifa ya uchaguzi (NEC) utakaochagua Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Wabunge na madiwani.