NA BAKAR MUSSA, PEMBA

WATENDAJI Tume ya Taifa ya Uchaguzi Tanzania (NEC), wametakiwa kuwa makini katika kusimamia majukumu yao kwa kuzingatia katiba na sheria za nchi, hali ambayo itafanikisha vyema zoezi la uchaguzi mkuu.

Akizungumza na wasimamizi na wasaidizi wa uchaguzi wa Tume hiyo wakati wa ufunguzi wa mafunzo kwa watendaji hao, Makamu mwenyekiti wa NEC, Jaji mstaafu, Mbarouk Salim Mbarouk, alisema kuna umuhimu kwa watendaji hao kuhakikisha wanasimamia vyema majukumu yao.

Alieleza uchaguzi ni mchakato unaojumuisha, hatua na taratibu mbali mbali na kwamba kufuatwa kwa taratibu hizo kama inavyotakiwa ndio msingi wa kuuwezesha uchaguzi kuwa huru na wa haki.

Jaji Mbarouk alisema endapo watendaji hao watakiuka sheria na taratibu lazima zoezi la uchaguzi litaharibika na yatarajiwe kutokea kwa malalamiko ama vurugu.

Aliwaeleza watendaji hao kuelewa kuwa wameaminiwa na kwamba kuteuliwa kwao pamoja na mambo mengine imebainika kuwa na uwezo utakaofanikisha kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi.

Alisema ili waweze kutekeleza vyema majukumu yao lazima wajiamini na wavishirikishe vyama na wadau wengine wa uchaguzi kwa mambo yanayowahusu, hivyo taifa linawategemea katika kuifanikisha vyema kazi hiyo.

“Washirikisheni wadau wa uchaguzi na vyama vya siasa kwa lile linalowahusu, hatua ya kushirikishwa katika yale wanayoyaamini itaondosha malalamiko”, alisema.

Makamu Mwenyekiti huyo wa NEC, alifahamisha kwa mujibu wa katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ibara ya 74 (6), Tume hiyo imepewa jukumu la kusimamia na kuratibu uendeshaji wa uchaguzi wa rais na wabunge wa Jamhuri ya Muungano na madiwani kwa Tanzania bara.

“Na huku Zanzibar kwa ibara hiyo hiyo Tume hii imepewa jukumu la kuendesha na kusimamia uchaguzi wa rais wa Jamhuri ya Muungano na wabunge pekee, hivyo kazi hii mnaifanya kwa mujibu wa sheria za nchi”, alisema.

Kwa upande wake Mkurugenzi Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) Ofisi ya Zanzibar, Hamidu Mwanga akitowa mafunzo hayo aliwataka watendaji hao kuelewa kwamba wao ni muhimu katika utekelezaji wa kazi hiyo kwani ndio wanaoweza kufanikisha uchaguzi huo wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuwa huru, salama na kuaminika kwa watu wote na kutopelekea kuharibika ama kufutwa.

Alisema ni vyema watendaji hao kujitathmini kwanza ili wasiweze kuharibu kazi hiyo kwani watakapoharibu sio wataitia doa Tume pekee bali watasababisha serikali kuitia hasara ya kufanya uchaguzi mwengine jambo ambalo halipendezi kutokea.

Aidha mkurugenzi huyo aliwataka watendaji hao kuwa makini katika kutekeleza majukumu waliyopewa na kujaribu kuwa na lugha nzuri kwa watu wanaowahudumia.

“Kuweni na lugha nzuri ili ziweze kuwavutia wananchi na wale mtakao waongoza kufanya kazi hii, kwa kuweka mbele ushirikiano katika kufanikisha kazi hii muhimu kwa taifa na kuiletea sifa nchi yetu”, alisema.

Hamidu, aliwasisitiza watendaji hao kuachana na ushabiki wa vyama vya siasa wakati wakiwa watumishi wa NEC na kwa yule mwenye sare za Chama chochote cha siasa aziweke pembeni mpaka utakapomalizika.

Hata hivyo aliwataka kutokubali kuyumbishwa na watu wengine pale wanapotaka kutoa maamuzi ya utekelezaji wa majukumu yao kwani wao ndio wenye dhamana kubwa kwa mujibu wa sheria wakati huo.