NA ABOUD MAHMOUD

KLABU ya soka ya Jamhuri iliyoshuka daraja msimu uliopita na kucheza ligi daraja ya kwanza kanda ya Pemba,imesema imepeleka barua ya malalamiko kwa kamati ya rufaa.

Kauli hiyo imetolewa na meneja wa klabu hiyo, Abdullah Abeid ‘Elisha’ alipokuwa akizungumza na mwandishi wa habari hizi kwa njia ya simu.

Alisema kwamba barua waliyoipeleka kwa kamati hiyo inahusiana na malalamiko ya kulipishwa faini ya shilingi milioni 2.

“Mpaka hivi sasa tupo tunasubiri kamati ya rufaa itakavyoamua juu ya malalamiko yetu tulioyapeleka ya kudaiwa kulipa faini ya fedha hizo kwa mechi mbili,”alisema.

Elisha alisema kitendo kilichoifanya klabu yake kutozwa faini hiyo sio cha ukweli na alibainisha kwamba, kutokea vitendo hivyo kunatokana na wachezaji kuchoka kwa sababu walikuwa na mechi za papo kwa papo.

Alisema taratibu za mchezo wa soka wanazijua na hawawezi kufanya vitendo vya utovu wa nidhamu kwa kuharibu mchezo kwa makusudi.

“Hatuwezi kufanya vitendo visivyoeleweka sisi tunafahamu nini tunachokifanya, siku ya tukio wachezaji wetu walikuwa wamechoka sana na ukiangalia walikuwa na mechi za hapo kwa hapo,”alifahamisha.

Aidha Meneja huyo alisema klabu hiyo inatarajia kufanya mkutano wa pamoja hivi karibuni, kwa kuwashirikisha wanachama, mashabiki na wapenzi wao kwa ajili ya kufanya tathmini ya ligi iliyopita na kujipanga kwa ligi daraja la kwanza.

Alieleza moja ya sababu zilizofanya Jamhuri kushuka daraja ni kupungua kwa mashirikiano kutoka kwa wanachama na wapenzi wake, hivyo amewaomba kukaa pamoja ili kurejesha mashirikiano hayo.