NA SIMAI HAJI, MCC

JANA wazanzibari walikamilisha sherehe za Eid el Hajj ambapo serikali ya Mapinduzi Zanzibar imeruhusu kufanyika sherehe hizo kwenye viwanja mbalimbali vya kufurahishia watoto baada ya kupungua kwa ugonjwa wa corona.

Sikuku ya Eid El Fitri inayofanyika mwezi wa mfungo mosi haikuwa na sherehe kutokana na kuweko kwa ugonjwa wa corona.

Hivyo basi kipindi chote cha corona tuliiona jamii ikichukua tahadhari kubwa ili kuona kuwa hakuna maambukizi mapya.

Kwa mujibu wa watalamu wa afya wanasema kuwa ugonjwa wa corona utachelewa sana kumalizka lakini kwa Tanzania hatuna budi kumshukuru Mwenyezi Mungu kutupunguzia sana maambukizi ya ugonjwa huo.

Hata hivyo, kupungua kwa maradhi haya kusitupe mwanya wa kusahau ushauri uliotolewa na wataalamu wa afya kwani kufanya hivyo kunaweza kusababisha tatizo jengine na kwamba jamii bado inatakiwa kuchukua tahadhari.

Mbali na kuruhusiwa sherehe hizi za sikukuu, lakini pia shughuli mbalimbali za kijamii kwa sasa zimeruhusiwa na kwamba watu wanafanya shughuli zao kama kawaida ila la msingi ni kuendelea kuchukua tahadhari.

Miongoni mwa mambo yaliyoruhusiwa ni pamoja na kufunguliwa skuli zote kuanzia ngazi ya maandalizi, msingi, sekondari na vyuo vikuu.

Mambo mengine ni shughuli za michezo kwenye viwanja mbalimbali, burudani na matamasha, shughuli za harusi na mazishi, kufanya ibada na hata madrasa.

Kama serikali ilivyotoa miongozo kwenye shughuli zote z hizo za kijamii na kiserikali bado watu wanatakiwa kuchukua tahadhari ili kuona kwamba hakuna tena maambukizi mapya ya ugonjwa huo hapa Zanzibar.

Mgonjwa wa kwanza wa corona hapa Zanzibar aliripotiwa Machi 17 mwaka huu na hivyo kulazimika kufungwa shughuli zote za kijamii na baadhi ya serikali ili kuona kwamba maambukizi ya ugonjwa huo yanadhibitiwa.

Aidha nchi ya China ambayo ndio kitovu cha ugonjwa huo, iliripoti maambukizi hayo Disemba mwaka jana na hadi sasa karibu nchi nyingi duniani zimethibitisha kupata wagonjwa wenye maambukizi ya corona.