BIASHARA haramu ya dawa za kulevya imekuwa ikiumiza vichwa vya viongozi wa nchi mbalimbali duniani pamoja na wananchi wasiopenda iendelee kushamiri.

Nguvu na fedha nyingi zimekuwa zikitumika katika kupambana na wanaofanya biashara hiyo ambayo kwa kweli haina manufaa yoyote kwa vijana wanaotumia mihadarati hiyo.

Tangu kuibuka kwa uraibu huu unaowaingizia fedha nyingi wanaofanya biashara ya kuusambaza, nchi nyingi zimekuwa zikilia kwa jinsi nguvu kazi zao zinavyoteketea kila uchao.

Yumkini kushamiri kwa biashara na matumizi ya dawa haramu za kulevya hapa nchini, kunachangiwa zaidi na rushwa muhali kwani katika nchi ndogo kieneo kama Zanzibar, haiwezekani wanaoingiza sumu hiyo wawe hawajulikani walipo na namna wanavyoendesha shughuli zao hizo.

Kila baada ya siku kadhaa tunasikia jeshi la polisi limekamata vijana wanaotumia dawa hizo mitaani ama kwa kunusa au kujidunga, tena hawa hushikwa kwa kuwa wengi wao wamemalizika kiafya na hawana tena uwezo hata wa kukimbia ili kujitetea.

Hawa ni wale wanaoitwa wateja, ambao wengine miongoni mwao pia hutumiwa na wanaoingiza ‘unga’ nchini kwa kuwasambazia vijana wenzao kwa ujira mdogo.

La kujiuliza sasa, kuna tatizo gani linalokwamisha kukamatwa vigogo wakuu wa mihadarati ambao ndio shina, na badala yake tunaishia kuganga matawi?

Iliwahi kutolewa orodha ya majina ya watu wanaosadikiwa kuingiza nchini dawa hizo, au bora tuziite sumu maana kazi ya dawa ni kutibu, lakini hizi zinaua taratibu.

Tunaelezwa wapo vijana wengi wa kitanzania katika magereza ya ughaibuni ikiwemo Afrika Kusini na China wanaotumikia vifungo vya miaka mingi baada ya kubambwa na kilo za ‘sumu’ za kulevya.

Wengine wanashikwa wakitoka nazo katika nchi za ng’ambo kabla hawajafika nazo huku Afrika, lakini hakuna ubishi kwamba baadhi yao hupita nazo katika viwanja vyetu na wala hawashikwi.

Hapa Zanzibar kuna mitaa inayofahamika na kila mtu kwa kuwepo ‘maduka’ yanayouza dawa za kulevya ambazo haziingizi kodi serikalini kutokana na uharamu wake.