WATAALAMU wanasema michezo ya watoto ni yale matendo yote yanayofanywa na watoto, kwa lengo la kujifurahisha na kupata utoshelevu wa mazoezi ya kimwili na kiakili.

Hii ni kusema michezo ya watoto ni harakati za kila siku wazifanyazo ili wapate furaha kimwili na kiakili. Michezo imegawnyika katika makundi mawili. Ile ya kijadi na pia ipo michezo ya kisasa.

Michezo ya jadi ni michezo yote iliyopo katika jamii tangu zamani. Mifano ya michezo hiyo ni pamoja na kobole, nage na ukuti na mengine mingi.

Michezo ya kisasa ni ile yote ambayo kwa hakika haina asili ya jamii zetu. Hata hivyo michezo yote ina sifa zinazofanana ikiwemo ile inayozingatia umri husika wa watoto.

Wataalamu wa masuala ya michezo ya watoto wamekuwa wakizungumzia umuhimu wa michezo katika maendeleo ya kielimu na kiafya na mara zote wanasisitiza haja ya kujengewa mazingira bora kwa ajili ya kushiriki michezo.

Kwa kufahamu umuhimu wa michezo kwa watoto, serikali imekuwa mstari wa mbele katika kuhakikisha fursa za michezo kwa watoto zinapatikana na tayari imeamua kurejesha michezo maskulini ambako huko ndiko kunakoibuliwa vipaji mbalimbali.

Lakini pamoja na azma hiyo njenye, hivi sasa kumejitokeza wimbi la uvamiaji wa maeneo ya wazi ambayo watoto huyatumia kwa ajili ya michezo yao kwa kuegeshwa magari au kutumika kinyume na mipango iliyokusudiwa.

Jambo hilo si sawa hata kidogo na halihitaji serikali kuu kulikomesha, bali jamii yenyewe zinapaswa kulikemea hili na kutokuwa tayari kulifumbia macho.

Hali hiyo imekuwa ikiwanyima watoto fursa ya kushiriki michezo ikizingatiwa bado Zanzibar hatujatenga maeneo maalumu kwa ajili ya watoto kushiriki michezo.

Kutokana na hali hiyo, watoto hulazimika kuvitumia viwanja vya michezo nyakati za mchana pekee huku jua kali likiwaka na hivyo kuwaweka katika mazingira magumu.

Kutokana na hali hiyo, tungelipenda kuchukuwa fursa hii kuvitaka vyombo husika kufikiria namna ya kuandaa maeneo ambayo yatatumiwa na watoto kwa ajili ya michezo yao badala ya hali iliyopo sasa.

Kufanya hivyo tutakuwa tamewasaidia watoto katika kuwajengea mustakabali wao wa baadaye kupitia michezo na kwa kufanya hivyo, tutatoa fursa kwa watoto kucheza katika mazingira salama.

Maeneo kama hayo ni muhimu kwa vile yatatumiwa na watoto kucheza kwa pamoja na hata utaratibu wa kuviona vipaji vyao utakuwa umerahisishwa.

Kinachohitajika ni kujipanga kwa mabaraza yetu ya mitaa na halmashauri kwa kuandaa meneo kama hayo na kuyahifadhi na matumizi yalio nje ya malengo.

Pamoja na changamoto nyingi zinazoikabili sekta ya michezo, lakini, bado tuna nafasi ya kuiimarisha ikiwa kila mmoja wetu atatimiza wajibu wake.