NA GASPARY CHARLES
JAMII imetakiwa kuendelea kufuata taratibu na maelekezo ya wataalamu wa afya, juu ya kujikinga na virusi vya corona.
Wito huo ulitolewa na Dk. Abdalla Omar Hassan, katika kikao cha vijana waelimishaji jamii juu ya utoaji wa elimu ya kujikinga na virusi vya corona, kutoka wilaya ya Micheweni kilichoandaliwa na Jukwaa la Vijana Zanzibar (ZYF).
Alisema licha ya mafanikio yaliyofikiwa nchini ya kupambana na virusi hivyo, bado kunahitajika juhudi za makusudi kwa kila mmoja kuhakikisha anaendelea kuchukua tahadhari zaidi na kufuata malekezo yote yanayotolewa na wataamu wa afya.
“Kila mmoja kwa nafasi yake anatakiwa kuendelea kuhakikisha anazingatia kanuni zote za usafi, kwani bado hatujahakikishia kuimaliza kabisa corona,” alisema.
Aidha aliwaomba vijana kuendelea kuwa msitari wa mbele katika utoaji wa elimu ya kujikinga na corona, kwani elimu hiyo bado inahitajika zaidi kutolewa kwa makundi mbalimbali ndani ya jamii.
“Tuweke utaratibu wa kuwa na taarifa mpya na sahihi kuhusu virusi hivi ili tutoe elimu hii kwa makundi yote yaliyo katika jamii zetu,” alisema.
Kwa upande wake, mmoja wa washiriki wa kikao hicho, Abdalla Ali Said alisema licha ya kuwepo kwa mafanikio hayo lakini wataendelea kutoa elimu kwa jamii ili kuhakikisha kila mmoja nakua na elimu sahihi ya kujikinga na virusi hivyo.