HIVI karibuni miji ya Hiroshima na Nagasaki iliyoko nchini Japan iliadhimisha miaka 75 tangu yalipodondosha mabomu ya atomiki na kusababisha vifo na majeruhi ya halaiki.

Marekani ilidodosha mabomu hayo katika miji hiyo na kusababisha Japan kusalimu amri na kumalizika kwa vita vya pili vya dunia mnamo mwaka 1945.

Marekani ilidondosha bomu la kwanza la nyuklia katika mji wa Hiroshima Agosti 6 mwaka 1945 na kuwaua watu 140,000, idadi hiyo inajumuisha wale walionusurika mlipuko na kufariki baadae.

Siku tatu baadae Marekani ikadondosha bomu jingine katika mji wa bandari wa Nagasaki na kuwaua watu 74,000.  Siku sita baada ya mashambulizi hayo ya Marekani, Japan ilisalimu amri mnamo Agosti 15, 1945 na kuhitimisha vita vya pili vya dunia.

Majira ya saa mbili na robo asubuhi ya tarehe 6 Agosti 1945, ndege ya kijeshi ya Marekani chapa B-29 Enola Gay iliangusha bomu lililopewa jina la “Mvulana Mdogo” na kuwauwa hapo hapo watu 140,000 kati ya wakaazi 350,000 wa mji huo.

Maelfu ya watu wengine walikufa siku za baadaye kutokana na majeraha waliyopata na kuathirika na mionzi ya atomiki iliyotokana na mripuko wa mabomu hayo katika mji hiyo.

Kwa mujibu wa taarifa za kitabibu watu wengi walioathirika na mabomu waliofariki baadae waliathirika zaidi na magonjwa ya saratani kutoka na mionzi iliyotokana na miripuko hiyo.

Kwa muda wa miaka 75, tangu Marekani ilipodondosha mabomu hayo haijawahi hata mara moja kuomba msamaha kwa kupoteza maisha ya raia wasio na hatia kwenye mashambulizi hayo ya nyuklia iliyoyafanya.

Wanahistoria wengi wa magharibi wanaamini ilikuwa lazima kuhitimishwa kwa vita na kuepuka uvamizi ambao ungekuwa wa gharama kubwa zaidi.

Pamoja na mataifa mengi hivi sasa kuendelea na shughuli za utengenezaji wa silaha za nyuklia, lakini Japan imekuwa nchi ya kwanza duniani kushambuliwa kwa silaha za nyuklia.

Waziri mkuu wa Japan Shinzo Abe amerejelea ahadi yake kwamba Japan itaongoza juhudi za jumuiya ya kimataifa za kufikia ulimwengu usio na silaha nyuklia.

Mahudhurio ya mwaka huu yalikuwa asilimia 10 tu ya mahudhurio ya kawaida, ambapo viti vilitenganishwa vya kutosha huku watu wakiwa wamevaa barakowa.

Watu pekee walioruhusiwa kuhudhuria kumbukumbu hizo ni manusura wa mashambulizi hayo yaliyofanywa na Marekani pamoja na familia zao.

Abe aliweka shada la maua katika eneo hilo la kumbukumbu kuwaenzi waathirika wa mabomu hayo na kutoa hotuba, huku akisisitiza umuhimu wa ulimwengu usio na silaha za kemikali.

“Maafa yaliyoipata Nagasaki na Hiroshima na madhila yaliosababishwa na bomu hayo kwa watu wake lazima yasijirudie tena sehemu nyengine yoyote duniani”, alisema Abe katika hotuba yake hiyo.

“Ikiwa ni nchi pekee iliyoathiriwa na silaha za nyuklia wakati wa vita, ujumbe huu utaendelea kutobadilika katika taifa letu ili tuweze kusonga mbele hatua kwa hatua juhudi za jumuiya ya kimataifa kufikia hali ya kutokuwepo silaha za nyuklia duniani.

Meya Tomihisa Taue wa Nagasaki alisema Japan inakaribia kufikia enzi mpya ikiwa na manusura wachache vikongwe wa mashambulizi hayo wanaoweza kuwasimulia kizazi cha sasa historia yao.

Meya huyo alitaka ukweli huo kuchukuliwa kama indhari kwamba dunia inapaswa kuishi bila ya silaha za kinyuklia. “Nadhani ni jambo la kimaumbile kwa Japan, taifa pekee lililowahi kupata uzoefu wa kupigwa bomu la nyuklia, kudhamiria kuwa na dunia isiyo na silaha za nyuklia”, alisema meya huyo.

Taue alisema ukweli ni kwamba Japan iko chini ya mwamvuli wa nyuklia wa Marekani njia moja mahsusi ya kuondokana na hali hiyo na kufikia dunia isiyo silaha za nyuklia ni dhana ya kuwa na eneo lisilo nyuklia.

“Kama nchi ambayo imepitia kihoro cha silaha za nyuklia, tafadhali wekeni saini katika mkataba unaopiga marufuku silaha za nyuklia na hakikisheni inapata maridhiano mapema iwezekanavyo”, alisema Taue.

Meya Kazumi Matsui wa Hiroshima alisema kwamba ni kuzuka kwa hisia kali za utaifa ndiko kulikopelekea vita vya pili vya dunia na mabomu ya atomiki, jambo ambalo halipaswi tena kuachwa likarejea.

“Jamii iliyostaarabika inapaswa kuukataa uzalendo uliojikita kwenye ubinafsi na uungane dhidi ya vitisho vyote,” alisema meya huyo.

Katibu mkuu wa Umoja wa Kimataifa Antonio Guterres katika ujumbe wake uliosomwa na msaidizi wake Izumi Nakamitsu, ameonya kwamba matarajio ya silaha za nyuklia kutumika kwa makusudi, au kwa bahati mbaya ni hatari sana.

Terumi Tanaka ambaye sasa ana umri wa miaka 88, wakati shambulizi hayo yanatokea akiwa na umri wa miaka 13, anakumbuka kila kitu kilivyokuwa cheupe wakati wa maripuko huo.

Aliongeza kuwa, “niliona watu wengi waliokuwa wameungua na kujeruhiwa wakiondolewa, wale waliokuwa wamefariki tayari katika skuli ya msingi iliyogeuzwa kuwa malazi ya waliofariki na majeruhi”, alisema

Makamu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa na Mwakilishi wa ngazi ya juu wa masuala ya kusitisha silaha za maangamizi Izumi Nakamitsu, alisema katika ujumbe wake katika kumbukumbu ya Nagasaki Peace Memorial alisema dunia lazima irejee katika uelewa ya kuwa katika vita vya nyuklia hakuna anayeshinda na lazima visitokee.

Kumbukumbu ya miaka 75 inakuja wakati wasiwasi ukizidi kuongezeka juu ya kitisho cha nyuklia kutoka Korea Kaskazini na kuzidi kwa mivutano baina ya Marekani na China juu ya masuala kadhaa ikiwemo usalama na biashara.