KWA muda sasa taifa la Mali lilipo kaskazini mwa bara la Afrika limekosa utulivu wa kiusalama na kiuchumi na kusababisha wananchi wa nchi hiyo kuandamana kuipinga serikali ya nchi hiyo.

Taifa hilo linakabiliwa na waasi wa kiislamu ambao wanapambana wakiwa na silaha, lakini inasemekana nchi hiyo inakabiliwa na mdororo mkubwa wa kiuchumi.

Rais Ibrahim Boubacar Keïta aliingia madarakani mwaka 2013, na hivi sasa amekuwa madarakani kumalizia awamu yake ya pili kabla ya Agosti 18 mwaka 2020 wanajeshi waasi kufanya mapinduzi.

Wananchi wana mtuhumu Keita kusababisha hali ngumu ya uchumi na kushindwa kuyazuia makundi ya wapiganaji wa kiislamu ambayo yameiweka rehani amani ya nchi hiyo.

Kwa mujibu wa taarifa kutoka mjini Bamako, wanajeshi waasi wamelazimika kumuondoa madarakani rais huyo, ambapo muda fupi baada ya kumuweka kuzuizini walimlazimisha ajiuzulu.

Akizungumza kupitia kituo cha utangazaji cha taifa ORTM, Keita alisema kuwa kujiuzulu kwake kunaanza mara moja na kwamba asingependa kuona damu inamwagika huku yeye akiendelea kubakia madarakani.

“Sitaki damu imwagike ili mimi kuendelea kubaki madarakani” na kuongeza kuwa, “Ikiwa vikosi vyenye silaha vinataka hili liishe kwa kuingilia kati, nina cha kufanya?” alisema Keïta.

Awali picha na video zilizosambaa kwenye mitandao ya kijamii zilionyesha msafara unaoaminika kuwa wa rais Keita na waziri mkuu Cisse uliokuwa umezingirwa na wanajeshi.

Kukamatwa kwa viongozi hao kuna litumbukiza taifa hilo ambalo tayari linakabiliwa na makundi ya wanajihadi na maandamano katika mgogoro mkubwa.

Kiongozi mmoja wa wanajeshi waasi aliyezungumza na shirika la habari la AFP kwa sharti la kutotajwa jina alisema kuwa “rais na waziri mkuu wako chini ya udhibiti wa jeshi baada ya kukamatwa katika makaazi ya Keita mjini Bamako.

Ofisa mmoja wa jeshi Sidi Gakao amethibitisha taarifa hizo alipozungumza na shirika la habari la DPA kwa njia ya simu akisema kwamba “rais na waziri wake mkuu wamekamatwa”.

Taarifa za kukamatwa viongozi wa serikali zilipokelewa kwa furaha na umati wa watu waliokuwa wamekusanyika katikati ya mji kwa ajili ya kushinikiza Keita kujizulu.

Jumuiya ya kiuchumi ya Afrika Magharibi (ECOWAS), Umoja wa Mataifa, Ufaransa, Umoja wa Ulaya na Umoja wa Afrika, zimelaani uasi huo na kuonya juu ya jaribio lolote la kubadili madaraka kinyume na katiba katika taifa hilo.

Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio Guterres ametaka kuachiwa haraka na bila masharti kwa rais Keita na Cisse wakati wanadiplomasia mjini New York wakisema Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa litafanya mkutano wa dharura kwa ajili ya kujadili hali nchini Mali.

Kauli kama hiyo ya kutaka Keita kuachiwa pia imetolewa na mwenyekiti wa Umoja wa Afrika Moussa Faki Mahamat.

ECOWAS kwenye taarifa yake, imewataka wanajeshi kurejea kwenye kambi na kujizuia dhidi ya kitendo chochote kinyume na katiba na kujaribu kutatua tofauti za kisiasa kupitia mazungumzo.

Kwa upande wake Umoja wa Ulaya umesema unalaani jaribio la mapinduzi nchini Mali na unakataa mabadiliko yasiyo ya kikatiba. Taarifa hiyo imeongeza kwamba hatua hiyo haiwezi kuwa suluhisho la mgogoro mkubwa wa kisiasa ambao umeikumba Mali kwa miezi kadhaa.

Hata hivyo, siku mbili kabla ya wanajeshi waasi kumuondoa madarakani rais Keita, ambapo milio ya risasi ilisikika katika kambi muhimu ya jeshi karibu na mji mkuu wa Mali Bamako.

Baadhi ya watu walieleza kuwa kusikika wa milio hiyo ya risasi ni ishara kwamba na hofu ya kuzuka kwa uasi katika jeshi la nchini hiyo.

Ofisa moja katika kituo hicho cha jeshi aliliambia shirika la habari la AFP kwamba milio hiyo ya risasi ilikuwa kitendo cha uasi na kwamba wanajeshi wengi hawafurahishwi na hali ya kisiasa na kuongeza kuwa wanataka mabadiliko.

Lakini ofisa mwengine katika wizara ya mambo ya ulinzi ya Mali, alisema hakuna uasi wowote uliokuwa unaendelea na kuongeza hata hivyo, kwamba serikali inafuatilia hali hiyo kwa karibu.

Vuguvugu lililopewa jina la Juni 5, kutokana na tarehe ya maandamano ya kwanza, linaekeza hasira kuhusiana na hali mbaya ya kiuchumi, rushwa iliyokithiri serikalini na mzozo wa wapiganaji wa itikadi kali unaogharimu maisha ya watu.

Kampeni ya vuguvugu hilo dhidi ya Keita iligeuka mzozo mwezi uliopita, baada ya watu 11 kuuawa katika makabiliano na vikosi vya usalama, katika muda wa siku tatu za machafuko kufuatia maandamano hayo.

Tangu wakati huo, kundi hilo limakataa juhudi za upatanishi na rais Keita mwenye umri wa miaka 75, na liliapa kuendelea na maandamano dhidi yake.

Upinzani mara kwa mara umetupilia mbali mapendekezo ya kumaliza mzozo wa Mali yaliowasilishwa na wapatanishi wa kimataifa na badala yake kutoa madai ya kumtaka Keita ajiuzulu.

Huku hay yakiendelea washirika na majirani za Mali walikuwa wakihaha kuepusha nchi hiyo kutumbukia tena katika machafuko.

Maeneo makubwa ya nchi hiyo tayari yako nje ya udhibiti wa serikali, ambayo inapambana kudhibiti uasi wa wanamgambo wa Kiislamu, uliozuka kwa mara ya kwanza mwaka 2012 na umegharimu maisha ya maelf ya raia.