NIAMEY, MALI

WANAJESHI waliofanya mapinduzi nchini Mali wamemtangaza kiongozi wao Assimi Goita kuwa Rais wa nchi hiyo.

Taarifa zaidi zilisema kuwa, baada ya kupita siku 12 tangu kuondolewa madarakani Ibrahim Boubacar Keita, wanajeshi waliofanya mapinduzi nchini humo wamemchagua kiongozi wao Assimi Goita kuwa Rais kwa ajili ya kuongoza kipindi cha mpito.

Kabla ya hapo Assimi alikuwa kiongozi wa Kamati ya Taifa ya Kijeshi iliyoundwa baada ya kuondolewa madarakani Rais Ibrahim Boubacar Keita.

Hayo yanajiri katika hali ambayo, Jumuiya ya Kiuchumi ya Nchi ya Nchi za Magharibi mwa Afrika (ECOWAS) imewataka viongozi wa mapinduzi ya kijeshi nchini Mali kukabidhi madaraka kwa serikali ya mpito ya kiraia mara moja na waitishe uchaguzi ndani ya kipindi cha mwaka mmoja

Takwa hilo la ECOWAS linakuja siku chache baada ya viongozi wa mapinduzi ya kijeshi huko Mali kuuambia ujumbe wa wapatanishi wa jumuiya hiyo mjini Bamako kuwa, wanataka kusalia madarakani kwa miaka mitatu ya kipindi cha mpito kabla ya kuitishwa uchaguzi.

Licha ya wananchi wa Mali kufurahishwa na kuondolewa madarakani Ibrahim Boubacar Keita, lakini nchi za eneo na hata asasi na jumuiya za kimataifa hazijafurahishwa na mapinduzi hayo na zinasisitiza kurejeshwa utawala wa kisheria katika nchi hiyo ya magharibi mwa Afrika.