AMMAN, JORDAN

WIZARA  ya Mashauri ya Kigeni ya Jordan imelaani vikali hatua ya utawala haramu wa Israel ya kuafiki ujenzi wa vitongoji vipya vya walowezi wa Israel huko mashariki mwa mji wa Quds

Msemaji wa Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya Jordan  Dhaifullah al-Fayez, alisema kuwa, hatua ya Israel ya kuafiki mpango wa ujenzi wa  nyumba zaidi ya 1,000 za Waisrael huko mashariki mwa mji wa Quds inapingana na sheria za kimataifa kama ambavyo inakiuka maazimio ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa.

Aidha alisema kuwa, hatua hiyo inadhoofisha fursa ya kuupatia ufumbuzi mgogoro wa Palestina kwa mujibu wa sheria za kimataifa.

Taarifa ya Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya Jordan ilieleza kuwa, Amman inataka Israel isitishe hatua zake zote zinazokiuka sheria kuhusiana na ujenzi wa vitongoji vya Israel  na hatua zake za kupora ardhi za Wapalestina.

Hivi karibuni Televisheni ya Israel ilitangaza kwamba mamlaka ya mji wa Quds iliafiki mpango uliopasishwa na Wizara ya Masuala ya Quds wa kujenga kitongoji kipya huko kaskazini mwa mji huo mtakatifu.

Mpango huo unasisitiza kuwa eneo lote la Quds (Jerusalem) Mashariki na Magharibi ni mji mkuu wa Israel, kinyume kabisa na maazimio ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa.