Zao la falsafa ya elimu bure ya mwaka 1994
Kisomo cha watu wazima chawakomboa wengi Zanzibar
NA MWANDISHI WETU
KILA ifikapo mwanzoni wa Septemba ya kila mwaka hujulikana kuwa ni wiki ya kimataifa ya kisomo cha watu wazima duniani – International Literacy Day (ILD) iliyotokana na mkutano mkuu katika kikao cha 14 cha shirika la elimu, sayansi na utamaduni la Umioja wa Mataifa yaani UNESCO mwaka 1966 kilichofanyika Tehran, Iran.
Tokea mwaka 1967 siku hiyo ya maadhimisho ya Elimu ya Watu wazima imekuwa ikifanyika duniani kote kila mwaka.
Pamoja na mambo mengine lakini lengo na madhumuni ya kuwakumbusha wananchi na jamii juu ya umuhimu wa kisomo cha watu wazima na elimu kwa ujumla kuwa suala la msingi, utu na haki ya kila mtu.
Pia juma hili, huwatanabahisha na kuwasisitiza wananchi na jamii kutilia mkazo suala la elimu kwa maendeleo endelevu katika jamii ili kuelekeza juhudi katika mahitaji ya fani na ujuzi wa kazi bila ya kujali changamoto zilizopo.
Maadhimisho ya siku ya Elimu ya Watu Wazima kimataifa mwaka huu ni fursa kubwa ya kuelezea umoja na mshikamano na kuwa ni mwaka wa lugha za asili au lugha za kienyeji sambamba na miaka 26 ya mkutano wa elimu maalum duniani.
Siku hiyo ya Elimu ya Watu Wazima duniani mwaka huu itaangalia zaidi namna ya elimu ya watu wazima inavyowafikia wale waliokuwa hawakusoma.
Vile vile siku hiyo kutajadiliwa suala la tabia na sifa za lugha mbalimbali katika dunia ya leo ya utandawazi pamoja na utekelezwaji wake kupitia sera ya kisomo cha watu wazima kwa ajili ya kufikia mafanikio ya mjumuisho ndani ya lugha tofauti.
Shirika la Elimu, Sayansi na Utamaduni ulimwenguni (UNESCO) limeitangaza juma la kisomo cha watu wazima ili kutoa mwamko na taaluma duniani kote juu ya masuala mtambuka yanayohusu elimu ya watu wazima na watoto.
Hii inaonesha jinsi shirika hili la Umoja wa Mataifa linavvyochukua nafasi yake tokea mwaka 1966 katika kutekeleza mpango wa malengo ya Maendeleo Endelevu uliofikia mwaka 2015. Siku hii inainaangazia mabadiliko na maendeleleo ya kisomo yaliyofikiwa duniani kote.
UNESCO ni kitivo kikuu cha kukuza na kushughulikia elimu duniani tokea mwaka 1946 na kimeitangaza siku hiyo ya kimataifa ya Elimu ya Watu Wazima kwa kushirikiana na serikali, mashirika yasiyo ya kiserikali, jamii na wataalamu wa elimu kote ulimwenguni.
Kwa kutumia kauli mbiu na mipango yake inawaweka katika hali ya tahadhari na kujaribu kubadilisha hali mbaya na kurudisha kiwango stahiki cha elimu kwa jamii.
Siku ya kimataifa ya kisomo cha watu wazima ni siku maalum ya kuwakumbusha viongozi, watu maarufu na jamii kwa ujumla juu ya hali iliyopo ya kisomo cha watu wazima na kujifunza.
Ukiangalia katika bango la UNESCO inatumia msemo wa ‘Kisomo ndio suluhisho sahihi’ kama ni ufunguo wa haki ya watu wote kupata elimu. Na hapa ndio katika mwaka 2015 Umoja wa Mataifa ilianzisha Malengo ya Maendeleo Endelevu kwa kuhamasisha juhudi za kupunguza umasikini na tofauti duniani.
Sambamba na siku hiyo UNESCO pia imetangaza tuzo za kimataifa za kisomo cha watu wazima mwaka huu kwa wale wanaofanya vizuri katika masuala ya uibuaji na ubunifu kwa kutumia kauli mbiu ya 2018 isemayo ‘Literacy and skills development’ ambayo imesaidia sana katika kujenga uelewa wa kisomo na kujifunza.
Hapa nchini Tanzania ikiwa ni miongoni mwa nchi zilizoridhia na kuikubali siku hiyo hufanya maadhimisho hayo maarufu kama Juma la Elimu ya Watu Wazima au wiki ya Elimu ya Watu Wazima kwa vile huadhimishwa kuanzia tarehe 1 hadi 8 ya Septemba kila mwaka.
Kama ilivyo kwa nchi nyingine sambamba na kusudio la UNESCO kuiweka siku hiyo serikali na taasisi za kielimu hufanya tathmini, kuangalia mafanikio na changamoto zilizopo kwa ajili ya kupanga mikakati mipya na kuchukua hatua za makusudi kuondoa changamoto hizo.
Mara nyingi Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali kupitia Idara ya Elimu Mbadala na Watu Wazima inakuwa mstari wa mbele katika kufanikisha suala la kutoa elimu kwa wananchi wote hapa Zanzibar kwa kuwapatia fursa hiyo kupitia mfumo usio rasmi ‘informal system’ kuanzia elimu ya msingi, sekondari, ufundi na hata elimu ya juu.
Kwa mukhtaza huo, tukiangalia hali ya kisomo cha watu wazima hapa nchini ni ya kuridhisha sana kulinganisha na miaka iliyopita kwani kwa sasa jumla ya wanakisomo zaidi ya 8,774 wakiwemo wanawake 7,639 na wanaume 1,135 wako madarasani Unguja na Pemba.
Mambo ya msingi ni kuhakikisha kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kupitia taasisi zake hasa Idara ya Elimu Mbadala na Watu Wazima kuhamasisha na kujenga uwelewa kwa wananchi kufahamu umuhimu wa siku hiyo na kujitokeza kwa wingi katika maadhimisho hayo ili waweze kujifunza wengi yanayopatikana katika elimu ya watu wazima.
Kama inavyoeleweka sehemu za vijijini katika visiwa vya Unguja na Pemba kuna baadhi ya watu hawajui kusoma wala kuandika jambo ambalo kwa maisha ya sasa ni jambo la aibu sana.
Hivyo, serikali haina budi kuhakikisha kuwa inalenga macho yake huko ili kuona kwamba inawatambua watu wasiosoma ili na wao waoate elimu kama raia wengine hapa nchini hasa ikizingatiwa kuwa elimu ni haki ya msingi ya kila raia.
Viongozi wa maneo kama vile masheha, wawakilishi, madiwani na wabunge washiriki kikamilifu katika kuwahamasisha wananchi wao kuhudhuria kisomo cha watu wazima hasa kwa wale wasiojua kusoma na kuandika.maadhimisho hayo.
Kama ilivyo kwa siku nyingine za kimataifa kuna umuhimu mkubwa kwa wamiliki wa vyombo vya habari hapa nchini kutilia kuweka mezani, kujadili na kutoa fursa kwa wahusika kuhamasisha siku hiyo kupitia vyombo vyao.
Idara ya Elimu Mbadala na Watu Wazima inawatakia wananchi na wanakisomo kote nchini kuona umuhimu wa elimu ambao ndio siri ya mafanikio ya mambo mbalimbali kwa dnia ya sasa na ijayo.
Fahamu kwa kumpatia mtoto elimu ni sawa sawa na nakshi katika jiwe kwani itampa msingi imara kufikia malengoi yake.
Hata hivyo wale ambao hawajapata elimu kwa sasa nao hawajachelewa kufikia malengo yao, kwani Serikali imeweka mfumo mzuri kuona watu wote wa Unguja na Pemba mkubwa na mdogo wanafaidika na elimu bure iliyotangazwa na Hayati Mzee Abeid Amani Karume mnamo mwaka 1964 falsafa ambayo inaendelea hadi leo.