NA ZUHURA JUMA, PEMBA

WANANCHI kisiwani Pemba, wametakiwa kudumisha amani, mshikamano na upendo walionao, katika kipindi cha kuelekea uchaguzi mkuu mwaka huu, ili kuepusha mifarakano ndani ya jamii.

Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake Katibu wa Kamati ya Maadili kutoka Jumuiya ya Maimamu (JUMAZA) Wilaya ya Chake Chake, Sheikh Abdalla Mnubi Abass alisema, kipindi wanachoelekea ni kigumu, hivyo ipo haja kuendelea kushikamana na kushirikiana katika mambo ya kijamii.

Alisema, si vyema kuzipa nafasi chuki, fitina na ufisadi, kwani zinajenga mfarakano na kuleta mpasuko ndani ya jamii, hivyo waendelee kudumisha amani na upendo katika kipindi chote cha uchaguzi mpaka kitakapomalizika, ili waishi kwa amani.

“Tusivunje udugu wala tusifarikiane kwa mambo ya siasa kwani ni jambo la kupita na sisi tutabaki kuwa wamoja tu, kwa hiyo kipindi kifupi cha uchaguzi tusikifanye kuwa cha migogoro”, alisema Mnubi.

Alieleza kila mmoja ana haki ya kuchagua kiongozi anayemtaka, hivyo si vyema kufanyiana chuki baada ya uchaguzi kwa sababu ya kupata kwa chama fulani.

“Tuishi maisha ya kupendane, kushrikiana na kushikamana, kipindi cha uchaguzi ni kipindi cha mpito, chagua kiongozi unaemtaka lakini tusifarakane”, alieleza Katibu huyo.